3512; Faida kabla ya mengine.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Watu huwa wanahangaika na mengi sana kwenye biashara.
Lakini yale ya msingi kabisa ambayo ni machache huwa hawayapi uzito mkubwa.
Moja ya mambo ya msingi ambayo yamekuwa hayazingatiwi kwenye biashara ni faida.
Watu hutumia muda mwingi sana kuhangaika ni biashara gani wafanye au waifanye kwa namna gani, lakini wanasahau kabisa kuhusu faida.
Biashara nyingi zimekuwa zinajiendesha bila ya faida na hilo ndiyo limekuwa linazizuia kukua.
Biashara nyingi huwa zinaonekana zinaenda vizuri pale zinapokuwa hazina majukumu makubwa.
Pale mfanyabiashara anapokuwa mwenyewe, hajaajiri na wala hana mikopo, mambo yanaonekana kwenda.
Ni pale biashara inapoanza kuwa na majukumu makubwa ndiyo inaanza kuyumba.
Biashara inapoajiri watu na kuhitajika kulipa mishahara au inapochukua mikopo na kupaswa kufanya marejesho, ndiyo shida huwa zinaanza.
Biashara huwa zinayumba sana pale zinapokuwa na majukumu makubwa.
Wengi hudhani matatizo hayo ndiyo yanaharibu biashara, lakini ukweli ni biashara tayari ilikuwa dhaifu kabla hata ya matatizo.
Hivyo basi, kabla hujachukua hatua ya kukuza biashara yako zaidi ya hapo ilipo sasa, ona kwanza faida.
Hakikisha unaweza kuikokotoa na kuiona faida kwa uhalisia wake kabisa.
Kisha kupitia faida hiyo ndiyo upange ukuaji.
Kama ni kuajiri basi uangalie mtu unayemwajiri atachangia faida kiasi gani na atalipwa kiasi gani.
Kama ni kuchukua mkopo basi uangalie mkopo huo utachangia faida kiasi gani na marejesho yatakuwa kiasi gani.
Ukijaribu kuchukua hatua za ukuaji kabla ya kuweza kuikokotoa na kuiona faida kwa uhalisia, utaishia kupata anguko ambalo litaharibu hata kile ambacho umeshakijenga.
Rafiki, je unaweza kukokotoa faida kwa usahihi na kuiona kwa uhalisia kwenye biashara yako?
Shirikisha kwenye maoni hapo chini na uitumie kuweka mipango ya ukuaji wa biashara yako.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe