Habari njema wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, kwenye eneo la maendeleo binafsi. Kupitia CHUO CHA MAUZO unapata fursa ya kujifunza kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea na kufanya mauzo makubwa zaidi.

Mafanikio kwenye maisha hayajali sana unajua nini, bali unamjua nani. Ni wale unaowajua na wanaokujua ndiyo wenye mchango mkubwa kwenye mafanikio yako. Ubora wa mahusiano yako na watu wengine una mchango mkubwa kwenye mafanikio yako.

Mahusiano bora na yanayoleta mafanikio makubwa ni yale ambayo ni ya muda mrefu. Mafanikio ya muda mrefu yanaleta hali ya kuaminiana na kushirikiana kwa karibu baina ya watu.

Kwenye mauzo, mahusiano yana nguvu kubwa sana. Kwani watu huwa wanakuwa tayari kununua kwa watu wanaowajua na kuwaamini. Watu wanaweza kuwa na uhitaji wa kitu, lakini wakashindwa kununua kwa kutokumjua na kumwamini muuzaji.

Hivyo kama unataka kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea na kufanya mauzo makubwa, kazana kujenga mahusiano ya muda mrefu na watu wengi zaidi kwenye maisha yako.

AINA YA MAHUSIANO YA KUJENGA.

Kuna mahusiano mengi ambayo tunayo kwenye maisha yetu. Mahusiano yote yana mchango kwenye mafanikio yetu, hivyo tunapaswa kuyajenga vizuri. Zifuatazo ni aina za mahusiano tunayopaswa kuyajenga na kuimarisha ili kufanikiwa.

Moja ni mahusiano na watu wa karibu kwetu. Hawa ni ndugu, jamaa na marafiki ambao unao. Watu hawa wana mchango mkubwa kwenye mafanikio yako pale wanapokuwa na imani kubwa kwako.

Mbili ni mahusiano na watu unaoshirikiana nao kwenye kazi au biashara unayofanya. Hawa wanaweza kukuonyesha fursa kubwa na nzuri kwako kufanikiwa kwenye kile unachofanya kama utakuwa na mahusiano mazuri nao.

Tatu ni mahusiano na wateja wako, hawa ndiyo wanaonunua kwako, hivyo unapokuwa na mahusiano mazuri nao wanaendelea kununua na kukuletea wateja wengine.

Wajibu wako ni kuhakikisha kila mtu unayekutana naye kwa namna moja au nyingine anaendelea kuwa sehemu ya mtandao wako. Unapaswa kuendelea kujenga mtandao wako kwa mahusiano ya muda mrefu, kwa sababu ukubwa wa mtandao wako ndiyo unaoamua ukubwa wa mafanikio yako.

MAMBO YA KUZINGATIA KWENYE KUJENGA MAHUSIANO YA MUDA MREFU.

Kwenye kujenga mahusiano ya muda mrefu ambayo yatakufanya kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa, zingatia mambo yafuatayo.

1. Wajue wengine kwa undani.

Mahusiano yanajengwa kwa kujuana na mahusiano bora ni yale ambayo watu wanajuana kwa undani. Ni wajibu wako kuhakikisha unawajua watu kwa undani ili kuweza kujenga na kuimarisha nao mahusiano. Kadiri unavyojua taarifa nyingi za watu ndivyo unavyokuwa na mambo mengi ya kujadiliana nao na pia kupata maeneo mengi ambayo mnafanana.

Kwa zama hizi za mitandao ya kijamii, ni rahisi sana kujua taarifa nyingi za watu kwa sababu wanaziweka wao wenyewe kwenye mitandao. Watu huwa wanashirikisha mambo muhimu kwao kama tarehe za kuzaliwa, watu muhimu, timu wanazoshabikia n.k. Wajibu wako ni kuwa mfuatiliaji na kukusanya taarifa kisha kuzitumia.

2. Weka mbele maslahi ya wengine.

Kwa kila jambo unalofanya, weka mbele maslahi ya wengine. Usifanye jambo kujinufaisha tu wewe mwenyewe bila kujali wengine wananufaikaje. Ufanye kuwa wajibu wako kuhakikisha kwamba kila mtu anayejihusisha na wewe anaondoka akiwa amenufaika na kuridhika. Hata kama ni kwenye majadiliano, usiangalie tu ushindi kwa upande wako, badala yake hakikisha upande wa pili pia umeondoka na ushindi.

Kwa watu wote unaojihusisha nao, jua maslahi yao ni nini kisha hakikisha unayatimiza. Usiridhike tu kukamilisha maslahi yako bila ya kujali ya wengine. Ukiwa na sifa ya wewe kupata unachotaka bila kujali wengine wamepata nini mahusiano yako na wengine hayatadumu muda mrefu. Watu watakuwa wanakukwepa kwa sababu wanajua unajijali wewe mwenyewe tu.

SOMA; Kuwa Bora Kwenye Majadiliano Ili Kuwa Muuzaji Bora Na Kufanya Mauzo Makubwa.

3. Mara zote fanya kilicho sahihi.

Ili kujenga mahusiano yatakayodumu kwa muda mrefu na kuwa na manufaa, mara zote fanya kilicho sahihi, hata kama hakuna anayeona. Kuna nyakati ambazo unajikuta kwenye hali ambayo unaweza kudanganya au kufanya kisicho sahihi na watu wasijue. Hata pale nyakati hizo zinapojitokeza, usizitumie kufanya yasiyo sahihi. Hiyo ni kwa sababu mwisho wa siku ukweli huja kujulikana. Inaweza kuchukua muda mrefu, lakini ukweli hujidhihirisha wazi. Na watu wanapokuja kugundua kwamba ulifanya ambacho hakikuwa sahihi, wanakosa imani na wewe.

Usitumie nafasi ya watu kutokujua kujinufaisha wewe zaidi kwa kufanya yasiyokuwa sahihi. Mara zote fanya kilicho sahihi hata kama watu hawajui. Watakuheshimu na kukuamini zaidi kwa kujua umefanya kilicho sahihi japokuwa ungeweza kufanya kisichokuwa sahihi na kujinufaisha zaidi.

4. Kuwa mshauri wa wateja wako.

Kwenye kujihusisha na wateja wako, usiishie tu kuwauzia, bali kuwa mshauri mzuri kwao. Washauri wateja wako kwa namna ambayo watapata matokeo bora kwenye kila jambo, hata kama itapelekea wewe kutokuwauzia. Kama kwa kuwashauri kwa usahihi wateja kutapelekea wewe usiuze, hujapata hasara, kwani watakuamini zaidi na imani hiyo itakupa mauzo makubwa na ya muda mrefu.

Usiishie tu kuwapa wateja kile wanachotaka kwa sababu utakamilisha mauzo, badala yake washauri kwa usahihi. Pale unapoona wanaweza kupata matokeo bora zaidi, chukua hatua ya kuwashauri namna hiyo. Hata kama itapelekea usiuze, usione umepoteza, bali ona umejenga kitu kikubwa kwa ajili ya baadaye.

5. Shirikiana nao nje ya biashara.

Kwenye kujenga mahusiano bora na wateja wako, unapaswa kushirikiana nao nje ya biashara unayofanya nao. Kila anayefanya biashara na wateja wako anaweza kuwahudumia vizuri kibiashara, ili kuonekana wa tofauti unapaswa kushirikiana nao hata nje ya biashara unayofanya nao. Hiyo unahusisha kuwasaidia kwenye mahitaji mengine wanayokuwa nayo na ambayo yako ndani ya uwezo wako. Na pia inahusisha wewe kushirikiana nao kwenye mambo ya kijamii ambayo yanawagusa wateja moja kwa moja.

Chukua hatua ya kushirikiana na wateja wako kwenye mambo mengine nje ya biashara unayofanya nao na hilo litaimarisha mahusiano yenu. Kadiri mteja anavyoona ukiwa na manufaa kwenye maeneo mengi ya maisha yake, ndivyo atakavyoendelea kuwa na wewe kwa muda mrefu na kukuletea wengine wengi.

Mauzo ni mahusiano, kadiri unavyojenga mahusiano imara na ya muda mrefu, ndivyo unavyokuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa. Kwa kuwajua wateja wako kiundani, kuweka maslahi yao mbele, kufanya yaliyo sahihi mara zote, kuwashauri vizuri na kushirikiana nao nje ya biashara utaweza kujenga na kudumisha mahusiano ya muda mrefu. Mahusiano hayo bora na ya muda mrefu yatakufanya kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.