3513; Wanachokimbia Wengine.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Wapo watu ambao wamekuwa wanalalamika kwamba fursa za kufanikiwa zimeisha.
Wapo wanaoamini fursa nzuri zote zimeshafanyiwa kazi na hakuna tena fursa mpya.
Lakini wengine wanaona fursa nzuri zimehodhiwa na wachache ambao wanajinufaisha nazo na kuwanyima wengine.
Mitazamo ya aina hiyo juu ya fursa ndiyo imekuwa kikwazo kwa wengi kunufaika na fursa ambazo bado zipo kwa wingi sana.
Ukweli ni kwamba fursa hazijaisha na wala hazitakuja kuisha.
Kila wakati kuna fursa nyingi mpya zinazozaliwa.
Na kadiri maendeleo yanavyokuwepo, ndivyo fursa zaidi zinazaliwa.
Njia moja ya kuziona fursa ni kuangalia kile ambacho kinapaswa kufanywa, lakini watu wanakwepa kukifanya.
Popote ulipo, unajua kabisa kuna kitu au vitu ambavyo vinapaswa kufanyika, lakini watu wengi hawapo tayari kuvifanya.
Na hawapo tayari kwa sababu ya ugumu wa kufanya vitu hivyo.
Na kwa sababu zipo njia rahisi za wao kupata wanachotaka, hawajisumbui na mambo magumu.
Kwa maana hiyo basi, kama unataka kuziona fursa nzuri, wewe angalia yale ambayo wengine wanakimbia kuyafanya.
Kama umeajiriwa, angalia majukumu ya kazini kwako, ambayo unajua kabisa yanapaswa kufanyika, lakini kila mfanyakazi anayakwepa.
Wewe yafanye majukumu hayo, bila ya kushurutishwa na mtu yeyote yule.
Kwa kufanya hivyo utafungua fursa kubwa na nzuri sana kwako, ambazo wengine hawatazipata.
Na unajua nini ambacho wengine watafanya baada ya wewe kupata fursa hizo?
Watakuchukia na kukusema una kiherehere na unataka uonekane unafanya kazi sana.
Nakupa ruhusa ya kuwapuuza na kuendelea kufanya yako.
Kadhalika kama unafanya biashara au mauzo, angalia ni vitu gani wateja wanataka ila watu hawataki kuwapa.
Wewe wape wateja kile wanachotaka kwa namna ambayo ni bora kwao na kwako.
Kwa kufanya hivyo utafungua fursa nyingi na kubwa.
Fursa zipo kwenye kazi ngumu ambayo watu wengi wanaikwepa. Ukiwa tayari kuikabili kazi hiyo ngumu, utaweza kufanya makubwa kwenye maisha yako.
Rafiki, ni kazi gani ngumu ambayo watu wamekuwa wanakwepa kuifanya kwenye shughuli unazofanya? Unahakikishaje unaifanya ili uweze kufungua fursa nzuri na kufanya makubwa?
Shirikisha kwenye maoni hapo chini ili uweze kufungua fursa nyingi kwa ajili yako.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe