Habari njema wauzaji bora kuwahi kutokea.
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya CHUO CHA MAUZO, yenye lengo la kutujenga kuwa wauzaji bora na kufanya mauzo makubwa.
Mkakati wetu mkuu kwenye CHUO CHA MAUZO ni kutengeneza wateja tarajiwa na kuwafuatilia wateja mara zote. Kwa kufanya hayo mawili, kufanya mauzo makubwa inakuwa ni matokeo ya uhakika.
Kutumia orodha mbalimbali ambazo zipo ni moja ya njia za kuweza kuwafikia wateja wengi zaidi na kuwafanya wajue kuhusu uwepo wa biashara. Orodha huwa zinakuwa na mawasiliano ya kuweza kuwafikia wateja moja kwa moja.
Kila biashara inapaswa kutengeneza na kutumia orodha yake kuwafikia wateja wengi zaidi na kuwafuatilia kwa msimamo wakubali kununua kwa mara ya kwanza na kuendelea kununua. Orodha ya biashara ni mgodi ambao ukijengwa na kutumiwa vizuri, biashara itaweza kunufaika sana.
Ili biashara iweze kupata ukuaji mkubwa, haiwezi kutegemea orodha yake peke yake. Maana hiyo inakuwa na ukomo wa watu waliopo na hata kama wanakuwa wanaongezeka, huwa siyo kwa kasi kubwa.
Hivyo biashara inapaswa kutafuta na kutumia orodha za watu wengine ili kuendelea kuwafikia watu wengi zaidi na kuwashawishi kuwa wateja tarajiwa na baadaye wateja.
Orodha za watu wengine, ambazo tayari zipo ni njia nzuri kwa kila biashara kutumia kufikia wateja wapya ambao bado hawajajua kuhusu uwepo wa biashara hiyo.

NJIA ZA KUTUMIA ORODHA ZA WENGINE KUWAFIKIA WATU WENGI ZAIDI.
Kuna njia mbalimbali za kutumia orodha za watu wengine kufikia watu wengi na kuwafahamisha kuhusu biashara. Baadhi ya njia hizo ni kama ifuatavyo;
1. Kununua Orodha.
Kuna watu ambao huwa wanakusanya na kuuza orodha zenye watu ambao wana sifa za aina fulani. Unaweza kutumia njia hii na kununua orodha ya watu ambao wana sifa za kuwa wateja wa biashara yako. Kwa kununua orodha unakuwa unaimiliki kabisa hivyo kuweza kuendelea kuwafuatilia wateja hao kwa muda mrefu bila gharama za ziada.
2. Kukodi Orodha.
Kuna watu huwa wanakuwa na orodha kubwa ya watu wenye sifa za aina fulani na huwa wanawakodishia watu wengine. Kwa njia hii unalipia kwa taarifa zako kutumwa kwenye orodha iliyopo na wale wenye uhitaji kuweza kukutafuta. Njia hii inakutaka urudie mara kwa mara ili kuweza kuwafikia na kuwashawishi watu wengi, kwa sababu siyo wote watashawishika kwa kusikia kuhusu wewe mara chache.
3. Kubadilishana Orodha.
Hii ni njia ya kubadilishana orodha na watu wengine ambao wana watu wenye sifa za kuwa wateja wako lakini siyo washindani wa moja kwa moja. Wewe unawapa nafasi ya kutumia orodha yako na wao wanakupa nafasi ya kutumia orodha yao. Kwa njia hiyo kila biashara inakuwa imepata nafasi ya kufikia wateja wapya ambao hawakuwa wanaijua awali. Njia hii haina gharama kwa sababu ni ya kubadilishana orodha.
Kwa njia hizo tatu, kila biashara inaweza kutumia orodha za watu wengine kuwafikia watu wengi zaidi na kati ya hao kuweza kupata wateja wapya tarajiwa.
SOMA; Tumia Orodha Mbalimbali Kufikia Wateja Wengi Zaidi.
MAMBO YA KUZINGATIA KWENYE KUTUMIA ORODHA ZA WENGINE ILI KUWA NA UFANISI.
Siyo orodha zote za wengine zina ubora sawa kwenye kupata wateja sahihi wa biashara. Hivyo ili kuhakikisha orodha unayotumia ni sahihi, zingatia mambo yafuatayo.
1. Jua sifa za watu waliopo kwenye orodha husuka.
Kabla ya kutumia orodha za wengine, jua kwanza sifa za watu waliopo kwenye orodha hizo. Angalia kama sifa za watu hao zinaendana na sifa za wateja tarajiwa unaowataka kwenye biashara yako. Hapa pia lazima uwe unajua sifa za wateja unaowalenga kwenye biashara yako ili uweze kuchagua orodha kwa usahihi.
2. Pima ubora wa orodha kabla ya kuitumia.
Watu wanaweza kueleza sifa nzuri za orodha walizonazo, lakini bado zikawa siyo sifa za kweli kama unavyotaka. Hivyo kabla ya kukubali kutumia orodha kwa makubaliano yoyote mnayoingia, pima kwanza ubora wa orodha husika. Kupima ubora wa orodha kunafanyika kwa kuchagua majina bila mpangilio wowote na kuwafuatilia ili kuona kama kweli sifa zinazoelezwa ni kweli. Ukishajiridhisha na ubora wa orodha, unaweza kuendelea na mpango wa kutumia.
3. Tumia orodha zaidi ya mara moja ili kupata wateja tarajiwa wengi.
Watu huwa hawasikii kitu kipya mara moja na kuchukua hatua hapo hapo, badala yake wanahitaji kusikia kitu kwa kurudia rudia ndiyo washawishike. Hivyo unapotumia orodha za wengine hakikisha unatumia zaidi ya mara moja ili kuweza kuwashawishi wengi. Hivyo hapa mpango mzuri ni kununua orodha kama ni bora na gharama unaweza kumudu. Kama hilo linashindikana basi kubadilishana orodha inaweza kuwa nafuu zaidi. Kukodi orodha inaweza kuwa na ukomo kwenye kuitumia na hivyo isiwe na matokeo mazuri. Lakini kama orodha ni kubwa na bora, kutumia mara kwa mara inakuwa na matokeo mazuri.
Orodha za watu wengine ambazo zina watu wenye sifa ya kuwa wateja wa biashara yako ni njia nzuri ya kuweza kuwafikia na kutengeneza wateja wapya tarajiwa wa biashara yako. Tafuta orodha hizo na kupata nafasi ya kuzitumia ili kufikia wateja wengi, iwe ni kwa kununua, kukodi au kubadilishana. Kabla ya kutumia orodha za wengine, hakikisha unajua ubora wake na kupata fursa ya kutumia orodha kwa muda mrefu ili kuweza kuwashawishi wengi zaidi.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.