3516; Kusubiri ruhusa.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Tulipokuwa watoto wachanga, tulikuwa tunajiamulia mambo yetu wenyewe na kwa namna tunavyotaka.
Tulipotaka kitu, tulilia mpaka tulipokipata, bila ya kujali chochote.
Kadiri tulivyoenda tukikua, wazazi na jamii ilitufundisha kuomba na kusubiri kupewa ruhusa kwenye kila kitu tunachotaka.
Zawadi na adhabu zilitumika kuhakikisha tunakuwa watu wa kuomba na kusubiri ruhusa.
Hilo lilifanikiwa na tukabadilika kutoka kuwa watu huru tunaojiamulia mambo yetu sisi wenyewe na kuishia kuwa watu tunaosubiri mpaka tupewe ruhusa.
Kijamii inaonekana ni ushindi, kwa sababu watu wengi wanatawalika.
Lakini kwa mtu binafsi ni kushindwa, kwa sababu mafanikio hayawezi kujengwa kwa kusubiri ruhusa.
Kama bado unasubiri mpaka watu wakupe ruhusa ndiyo ufanye mambo makubwa na ya tofauti, kamwe huwezi kufanikiwa.
Hiyo ni kwa sababu hayupo atakayekupa ruhusa ya kufanya mambo makubwa na ya tofauti.
Kwa sababu hao unaowasubiri wakupe ruhusa, wao wenyewe hawapo tayari kufanya mambo makubwa na ya tofauti.
Watu wote wanaokuzunguka wanafanya yale waliyozoea kufanya, ambayo ni madogo na ya kawaida sana.
Mafanikio makubwa hayawezi kutokana na kufanya mambo madogo na ya kawaida.
Kusubiri watu wakupe ruhusa ya kufanya mambo ambayo wao wenyewe hawapo tayari kufanya ni kujichelewesha kufanikiwa.
Wanaokuzunguka siyo tu hawawezi kukupa ruhusa ufanye makubwa na ya tofauti, bali watakuzuia kabisa usifanye.
Watakuonyesha jinsi kufanya unayotaka ni hatari kubwa kwako na ni bora kubaki kwenye mazoea ili uwe salama.
Hakuna anayependa kukuona wewe ukiwa unawazidi wao. Hivyo hawawezi kukuacha ufanye mambo ya tofauti na yaliyozoeleka.
Mafanikio yoyote makubwa unayoyataka kwenye maisha yako, unapaswa kujipa ruhusa wewe mwenyewe na siyo kusubiri wengine wakuruhusu.
Jipe ruhusa ukijua kabisa kwamba wengine hawatakuwa upande wako.
Hivyo unahitaji kuweka juhudi kubwa sana kwenye mengi ambayo utakabiliana nayo mpaka ufanikiwe.
Kujenga mafanikio yoyote makubwa unayotaka, usisubiri ruhusa ya mtu yeyote bali jipe ruhusa wewe mwenyewe.
Ruhusa yako inatosha kabisa kukuwezesha wewe kuchukua hatua unazopaswa kuchukua ili kufanikiwa.
Rafiki, ni maeneo gani umekuwa unasubiri wengine wakupe ruhusa ndiyo uchukue hatua kubwa kitu ambacho kimekuchelewesha?
Karibu ushirikishe kwenye maoni hapo chini ili uache kusubiri ruhusa kutoka kwa wengine na uchukue hatua sahihi kwako kufanikiwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe