3518; Asante, siyo muhimu.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Mafanikio makubwa kwenye maisha yako huwa yanaanza na ndoto kubwa.
Ni lazima uwe na ndoto kubwa sana, ambazo watu wote wanaona haziwezekani kabisa.
Lakini kuwa na ndoto pekee haitoshi, unahitaji kutengeneza taswira ya ndoto hiyo kwenye akili yangu.
Yaani utengeneze picha ambayo unajiona tayari umefikia ndoto kubwa uliyonayo.
Na hapo ndipo changamoto kubwa inapoanzia.
Utakapoweka picha ya ndoto yako kubwa kwenye akili yako, itaanza kukupinga.
Akili yako itakuonyesha kwamba hakuna namna unaweza kufikia ndoto hiyo kubwa.
Itakupa ushahidi kwamba unajidanganya tu.
Akili itaanza kukuletea maswali kama;
Unapanga kufikiaje ndoto hiyo?
Watu wengine watakuchukuliaje?
Wengine wameshindwa, kwa nini wewe uweze?
Hii inataka ujitese na kuumia sana.
Vipi kama ukishindwa?
Rafiki, akili itakuuliza na kukueleza mengi, ambayo yote huwezi kuwa na majibu yake.
Hivyo unapaswa kuwa na jibu moja ambalo utatoa kwa kila swali na maelezo.
Jibu hilo ni; “Asante, siyo muhimu.”
Hivyo tu, unaishia hapo, usitoe maelezo mengine ya ziada.
Hilo pia ndiyo jibu utakalowapa wale wote wanaokuambia ndoto zako haziwezekani au wanaojaribu kukubeza kwa namna yoyote ile.
Usihangaike kujieleza sana, kitu ambacho watu hawajawahi kuona hawawezi kuelewa.
Wewe wajibu kistaarabu; “Asante, siyo muhimu.”
Kisha endelea na mambo yako na waache wengine waendelee na mambo yao.
Kitu cha kwanza unachohitaji ni kuamini kwenye ndoto yako kubwa kwanza, hata kama hujui utaifikiaje.
Iamini bila ya shaka yoyote na usihangaike na chochote kinachokukwamisha.
Asili italeta kwako fursa kubwa na nzuri za kufikia ndoto hiyo.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com