Habari njema wauzaji bora kuwahi kutokea.
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya CHUO CHA MAUZO, yenye lengo la kutujenga kuwa wauzaji bora na kufanya mauzo makubwa.
Mkakati wetu mkuu kwenye CHUO CHA MAUZO ni kutengeneza wateja tarajiwa na kuwafuatilia wateja mara zote. Kwa kufanya hayo mawili, kufanya mauzo makubwa inakuwa ni matokeo ya uhakika.
Kwenye mauzo na maisha kwa ujumla, ukubwa wa mafanikio yako unategemea sana ukubwa wa mtandao wako. Haijalishi sana unajua nini au una nini, bali unamjua nani na nani anakujua.
Kuwa na mtandao mkubwa wa watu unaowajua na wanaokujua ni hitaji muhimu kwa kila mtu wa mauzo. Hiyo ni kwa sababu mambo yakiwa sawa, watu huwa wananunua kwa watu wanaowajua. Na hata mambo yasipokuwa sawa, bado watu wananunua kwa watu wanaowajua.
Matukio ya kujenga mtandao ni moja ya njia inayoweza kutumiwa na wauzaji kuweza kufikia wateja wengi zaidi na kwa muda mfupi. Hivyo kila muuzaji anapaswa kushiriki matukio ya kujenga mtandao akiwa na mkakati sahihi wa kuweza kufikia wateja wengi na kutengeneza wateja tarajiwa kwa ajili ya biashara yake.

Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza jinsi ya kutekeleza hilo kwa mafanikio makubwa. Karibu ujifunze.
AINA YA MATUKIO YA KUJENGA MTANDAO.
Matukio ya kujenga mtandao ni yale yanayowaleta pamoja watu wenye sifa za aina fulani. Pale watu wanaoshiriki matukio hayo wanapokuwa na sifa za kuwa wateja wa biashara fulani, inakuwa ni sehemu nzuri ya muuzaji kufikia wateja wengi kwa haraka na urahisi zaidi.
Baadhi ya matukio ya kujenga mtandao ambayo wauzaji wanaweza kushiriki ni kama ifuatavyo.
1. Mikutano na makongamano.
Haya ni matukio yanayowaleta watu wengi pamoja kwa ajili ya kupata taarifa au mafunzo ya aina fulani. Matukio ya aina hii huwa yanawaleta pamoja watu ambao wana sifa zinazoendana, kulingana na aina ya mkutano au kongamano. Pale watu wanaokuwepo kwenye mkutano au kongamano wana sifa za kuwa wateja wako, ni tukio muhimu la wewe kuwepo.
2. Mafunzo maalumu.
Haya ni mafunzo yanayokuwa yanafanyika kwa kipindi fulani na ambayo yanakuwa na washiriki wachache kuliko mikutano na makongamano. Kwenye mafunzo haya, washiriki wanakuwa na ushirikiano wa karibu zaidi kitu kinachowapelekea kujuana na kujenga mahusiano ya karibu. Muuzaji anaweza kushiriki mafunzo ya aina hiyo yenye wateja anaowalenga.
3. Michezo.
Michezo mbalimbali huwa inawaleta pamoja watu wanaoshabikia michezo hiyo. Watu hao wanakuwa na sifa zinazoendana ambazo pia zinawafanya kuwa wateja walengwa wa biashara za aina fulani. Muuzaji anaweza kushiriki matukio ya michezo yenye wateja anaowalenga.
4. Matukio ya uzinduzi.
Haya ni matukio ya uzinduzi wa vitu mbalimbali, inaweza kuwa ni biashara kuzindua bidhaa, huduma au tawi jipya. Inaweza kuwa pia kampeni mbalimbali zinazokuwa zinaendeshwa na taasisi mbalimbali. Muuzaji anaweza kushiriki matukio ya uzinduzi ambayo yanakuwa na wateja anaowalenga.
5. Uanachama.
Kuwa mwanachama wa vyama, taasisi au makundi ya aina fulani kunampa mtu fursa ya kujuana na wanachama wengine. Muuzaji anaweza kuwa mwanachama wa makundi ambayo yana wateja anaowalenga na kutumia fursa hiyo kuwafikia wengi na kutengeneza wateja tarajiwa.
Kama muuzaji angalia matukio mbalimbali yanayowaleta wateja unaowalenga pamoja na kuwa sehemu ya matukio hayo ili kufikia wateja wengi na kutengeneza wateja tarajiwa wengi.
SOMA; Jenga Mtandao Wako Ili Kuwa Muuzaji Bora Na Kufanya Mauzo Makubwa.
MAMBO YA KUFANYA KWENYE MATUKIO YA KUJENGA MTANDAO.
Ili kufikia wateja wengi zaidi na kutengeneza wateja tarajiwa ambao watafuatiliwa na kushawishiwa kuwa wateja kamili, kila muuzaji anayeshiriki matukio ya kujenga mtandao anapaswa kuzingatia mambo yafuatayo;
1. Kuvaa mavazi yenye nembo na jina la biashara.
Huwa kuna kauli inasema mwonekano wa kwanza ndiyo unaodumu kwenye kumbukumbu za watu. Hivyo unaposhiriki matukio ya kujenga mtandao, hakikisha jinsi watu wanavyokuona kwa mara ya kwanza inabaki kwenye kumbukumbu zao. Kufanikisha hilo hakikisha unavaa mavazi nadhifu na yenye nembo na jina la biashara yako. Ni rahisi watu kukujua na kukukumbuka kupitia mavazi unayokuwa umevaa.
2. Kuwa na kadi za biashara na vipeperushi.
Unaposhiriki matukio ya kujenga mtandao unapaswa kuwa na vitu unavyoweza kuwapa watu unaokutana nao ili waendelee kukukumbuka hata baada ya matukio na kupata mawasiliano yako kwa urahisi. Kuwa na kadi za biashara pamoja na vipeperushi ni njia rahisi ya kutekeleza hilo. Nenda kwenye matukio ya kujenga mtandao ukiwa na kadi za biashara na vipeperushi vya kutosha ili kugawa kwa wale unaokutana nao.
3. Kuwa na uwasilishaji mfupi wenye mvuto.
Andaa uwasilishaji mfupi, usiozidi sekunde 30 ambao unakuhusu wewe, unachofanya na manufaa ambayo watu wanayapata kwako. Sekunde 30 ndiyo muda wa juu kabisa unaoweza kupata na mtu kwenye matukio ya kujenga mtandao yanayohusisha watu wengi. Uwasilishaji wako mfupi unaweza kuwa kwa mfumo huu; Mimi ni …. (Jina lako) kutoka …. (Jina la biashara), tunawasaidia watu wenye …. (sifa ya wateja unaowalenga) kuweza ku …. (manufaa ambayo wateja wanayapata kwako na hawawezi kuyapata kwingine). Uwasilishaji huo unapaswa kutolewa kwa shauku kubwa ili kuwavutia na kuwashawishi wanaoupokea.
4. Kuongea na watu wengi zaidi.
Matukio ya kujenga mtandao yanapaswa kutumika kuwafikia watu wengi zaidi ndani ya muda mfupi. Unaposhiriki matukio hayo hakikisha unaongea na watu wengi kadiri iwezekanavyo. Ndiyo maana unahitaji uwasilishaji mfupi kuhusu wewe ambao utaweza kuutoa kwa haraka, kisha ukamjua mtu na mkabadilishana mawasiliano. Japokuwa hupaswi kuonekana ukiharakisha kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine, ni wajibu wako kuhakikisha umeongea na watu wengi zaidi na kuwapa uwasilishaji wako. Pia lenga kukutana na watu wote muhimu waliopo kwenye tukio husika, watu ambao watakuwa na manufaa makubwa zaidi kwako.
5. Kutafuta nafasi ya kuongea mbele ya wote.
Kwa matukio ambayo yana washiriki wengi na huwezi kuongea na wote mmoja mmoja, tafuta nafasi ya kuongea mbele ya watu wote ili usikike na wote walioshiriki. Nafasi za kutumia ni pale inapotolewa nafasi ya kujitambulisha mmoja mmoja, kuuliza maswali au kushirikisha mambo mbalimbali. Unapopata nafasi ya kuongea mbele ya wote, anza na uwasilishaji wako mfupi ili watu wakujue na wajue jinsi ya kunufaika na wewe, kisha ndiyo uendelee na kile unachotaka kuongea. Kwa kutafuta na kutumia fursa ya kuongea mbele ya wengine, washiriki wote wa tukio wanajua kuhusu wewe na wenye uhitaji kukutafuta wakati au baada ya tukio.
Unaposhiriki tukio lolote lenye wateja unaowalenga, hakikisha unaacha alama inayowafanya washiriki kukujua na kujua jinsi wanavyoweza kunufaika na wewe.
SOMA; Tumia Mtandao Wa Intaneti Kufikia Wateja Wengi Zaidi.
MAMBO YA KUFANYA BAADA YA MATUKIO YA KUJENGA MTANDAO.
Kushiriki matukio ya kujenga mtandao na kuwafikia wateja wengi ni hatua moja. Hatua nyingine muhimu sana ni ufuatiliaji unaofanyika baada ya kushiriki matukio hayo. Hatua hiyo ya ufuatiliaji ndiyo inayoamua kama ushiriki wa tukio umekuwa na manufaa au la.
Ili ushiriki wa matukio ya kujenga mtandao uwe wenye tija, mambo yafuatayo yanapaswa kufanyika baada ya kushiriki matukio hayo.
1. Ufuatiliaji ndani ya masaa 24.
Ndani ya masaa 24 baada ya kukutana na mtu kwenye matukio ya kujenga mtandao hakikisha unafanya ufuatiliaji wa kuwasiliana nao. Katika mawasiliano hayo, mtaje mtu kwa jina lake, jitambulishe jina lako na kumweleza mlikutana kwenye tukio mlilokutana kisha mkumbushe kitu ambacho kinawaunganisha pamoja kutoka kwenye tukio mliloshiriki. Kwenye ufuatiliaji huu wa kwanza usijaribu kuuza chochote, huu ni kwa ajili ya kuhakikisha unaendelea kukumbukwa, kwa sababu watu wanakuwa wamekutana na wengi hivyo inakuwa rahisi kusahaulika.
2. Kupata taarifa zaidi za waliofikiwa.
Watu unaokuwa umekutana nao kwenye matukio ya kujenga mtandao unakuwa na taarifa chache kuwahusu. Hivyo unapaswa kutafuta taarifa zaidi kuwahusu wao ili kuona namna bora ya kuendelea kushirikiana nao na kuwauzia. Hapo utaanza kwa kutafuta taarifa zao mtandaoni, kuwafuatilia kwenye mitandao ya kijamii na njia nyingine za kuwajua zaidi. Kadiri unavyopata taarifa zaidi utajikuta unawachuja watu na kuona wapi ambao watakufaa zaidi na wapi ambao hawatakufaa sana kwa kuanzia.
3. Kuomba miadi ya mawasiliano au kukutana.
Ukiwa umeshapata taarifa zaidi kuhusu watu uliowajua kupitia matukio ya kujenga mtandao, hatua inayofuata ni kuomba miadi ya mawasiliano au kukutana nao. Hapa ndipo unapoanza mchakato wako wa mauzo kwa kuwasilisha kile ulichonacho na jinsi kinavyoweza kuwanufaisha. Hii ni hatua muhimu sana kwenye ufuatiliaji wa watu unaokuwa umekutana nao kwenye matukio mbalimbali.
4. Kuwaingiza kwenye mchakato wa mauzo.
Baada ya kukutana na watu na kuwafuatilia, unawaingiza kwenye mchakato wa mauzo kulingana na kile unachouza na mahitaji wanayokuwa nayo. Utawasilisha kwao kile ulichonacho, thamani yake na manufaa wanayokwenda kupata. Utajibu mapingamizi mbalimbali waliyonayo na kuwashawishi wakubali kununua unachouza. Kwa kufuata mchakato wako hatua kwa hatua, utaweza kuwageuza wengi kuwa wateja kamili.
5. Kuwa na ufuatiliaji endelevu.
Watu wote unaokuwa umewajua kupitia matukio ya kujenga mtandao unapaswa kuendelea kuwafuatilia bila ya kuacha. Hata kama hawajafaa kuwa wateja wako, unapaswa kujenga, kukuza na kulinda mtandao wako. Kwani wao wanaweza wasiwe wateja, lakini wakawa wanawajua watu ambao ni wateja. Wajibu wako ni kuwa na mtandao mkubwa wa watu wanaokujua ili uweze kuuza kwa wengi zaidi. Endelea kuwafuatilia kwa mawasiliano, kukutana nao na kuendelea kushiriki matukio ya kujenga mtandao ambapo utaendelea kukutana nao.
Matukio ya kujenga mtandao ni sehemu nzuri ambayo kila muuzaji anaweza kuitumia kufikia wateja wengi na kutengeneza wateja tarajiwa. Chagua matukio ambayo yana watu wenye sifa za wateja unaowalenga, unaposhiriki hakikisha unawajua watu na wao wanakujua na baada ya kushiriki kuwa na ufuatiliaji ambao utaimarisha mtandao uliojenga na kutengeneza wateja wengi zaidi.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.