3521; Tafsiri ya kipato.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Kipato unachoingiza kwa sasa ni tathmini ya thamani ya ujuzi ulionao.

Kiasi cha fedha unachoingiza kinaendana na ujuzi ulionao.
Kipato hicho kinaeleza watu wanathamini ujuzi wako kiasi gani.

Hivyo kama kipato unachoingiza hakikutoshi, anza na thamani ya ujuzi ulionao.

Kuongeza kipato chako, anza kwa kuongeza thamani ya ujuzi ulionao.

Jifunze ujuzi wenye thamani kubwa zaidi na utaweza kulipwa zaidi.

Imezoeleka kwenye ajira kwamba kama mtu anataka aongezewe mshahara basi anaenda kuongeza elimu.

Kama alikuwa na cheti anaenda kuongeza diploma, kama alikuwa na diploma anatafuta digrii. Akiwa na digrii moja anaongeza nyingine n.k.

Ambacho wengi hawajui na hawazingatii ni kwamba hata kwenye kujiajiri na kufanya biashara, kuongeza kipato lazima uongeze elimu.

Uzuri ni elimu ya kuongeza kwenye biashara na kujiajiri siyo ya kurudi darasani.
Badala yake ni elimu ya kujifunza jinsi ya kufanya mambo ambayo kwa sasa huyafanyi au kama unayafanya siyo kwa viwango sahihi.

Ujuzi wa kukuza mauzo ni moja ya ujuzi ambao ukiuongeza utakuwezesha kukuza zaidi kipato chako.
Kujua njia bora za kupata wateja wengi zaidi, kuwashawishi wengi wakubali kununua na kuendelea kununua ni muhimu kuikuza biashara na kuongeza kipato chako.

Ujuzi wa kuajiri watu kwa usahihi utakuwezesha kuongeza kipato chako zaidi.
Kupata wafanyakazi sahihi, kuwapa mafunzi na kuwatunza kwa muda mrefu kwenye biashara itakuwezesha kuongeza kipato chako mara dufu.

Ujuzi wa usimamizi mzuri wa fedha za biashara ni muhimu kwenye kukuza kipato chako.
Kujua jinsi ya kupata mtaji kwa unafuu, kuongeza mzunguko wa fedha na kupata faida nzuri vitapelekea uweze kuingiza kipato kikubwa zaidi.

Unapokuwa huridhishwi na kipato unachoingiza, usilalamike wala kukata tamaa.
Badala yake anza na ujuzi ulionao sasa kwenye yale unayofanya.
Kisha chagua ni ujuzi gani unakwenda kuongeza ili uweze kuingiza kipato kikubwa zaidi.

Wekeza sana kwenye ujuzi wako mwenyewe na kwa timu yako ili uweze kuingiza kipato kikubwa zaidi ya unavyoingiza sasa.

Rafiki, kwa kipato unachoingiza sasa, ni ujuzi gani unapaswa kujijengea ili uweze kukikuza kipato hicho mara mbili?
Karibu ushirikishe kwenye maoni hapo chini na uende ukajijengee ujuzi huo ili ukuze kipato chako kwa uhakika.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com