3523; Kuwa ambavyo wengine hawataki.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Watu wamekuwa wanahangaika sana kutafuta siri za mafanikio, kama vile ni kitu ambacho kimefichwa.

Wanapoteza muda na fedha nyingi kutafuta siri hizo, wakati mambo yako bayana kabisa.

Wengi ambao hawajafanikiwa, wamezungukwa na wengine wengi ambao hawajafanikiwa.

Hivyo wanaona hawana hata watu wa kujifunza kwao, kwa sababu waliowazunguka hawajafanikiwa.

Ukweli ni kwamba siri za mafanikio hazijafichwa, bali zipo bayana kabisa.
Na pia unaweza kujifunza mengi kuhusu mafanikio kutoka kwa watu ambao hawajafanikiwa.

Kufanikiwa kwenye jambo lolote lile, siri kuu ni hii; KUWA VILE AMBAVYO WENGINE HAWATAKI KUWA.

Ulidhani siri ni nzito na iliyofichwa, lakini ukweli ndiyo huo.
Na uzuri wa siri hiyo ni tayari unao watu wa kukuonyesha nini unapaswa kuwa, kwa kwenda kinyume na walivyo wengi wanaokuzunguka.

Swali ni nini ambavyo wengi hawataki kuwa ambavyo wewe ukiwa utafanikiwa?

Vipo vingi, ila hivi vinne ndiyo vyenye nguvu zaidi.

Moja ni NIDHAMU.
Watu wengi hawana nidhamu, wanajiendea tu vile wanavyojisikia na hakuna hatua kubwa wanazopiga.
Wewe kuwa mtu mwenye NIDHAMU kali ya kupanga na kufanya kama ulivyopanga bila kujali unajisikiaje.

Mbili ni MAAMUZI.
Watu wengi hawafanyi maamuzi ya kile hasa wanachotaka. Matokeo yake wanajiendea tu na kila kitu kinachokuja mbele yao.
Wewe kuwa mtu wa MAAMUZI, ambapo ukishaamua jambo unakwenda nalo mpaka kulikamilisha kama ulivyopanga.
Usikubali kuwa mtu wa kuishia njiani kwenye yote unayoamua.

Tatu ni KAZI.
Kazi kubwa sana inahitajika ili mtu kujenga mafanikio makubwa anayoyataka.
Wengi hawapendi kuweka kazi, badala yake wanatafuta njia za mkato za kufanikiwa kwa haraka bila kuweka kazi.
Hicho ni kitu ambacho hakipo, hivyo wengi wanakwama kufanikiwa.
Wewe kuwa mtu unayependa KAZI, kuwa mchapa kazi hasa na utayapata mafanikio.
Usikubali yeyote akuzidi kwenye ufanyaji kazi.

Nne ni MSIMAMO.
Kuna watu huwa wanaonekana kuwa na sifa tatu zilizotangulia, wanakuwa na nidhamu, wanaamua vizuri na kuweka kazi. Lakini wanakuwa hawana msimamo kwenye ufanyaji wao. Kuna wakati wanafanya na wakati mwingine hawafanyi. Kupata matokeo makubwa bila ya msimamo inakuwa kitu kigumu.
Wewe kuwa mtu wa MSIMAMO mkali kwenye mambo yako yote.
Ukishaamua, unafanya kwa msimamo bila kuacha, hata ukutane na nini.
Msimamo utakupa mengi sana ambayo wengi wanayakosa.

Kwa kuleta vyote vinne kwa pamoja tunaweza kusema ili ufanikiwe, unapaswa kuwa na NIDHAMU KALI YA KUAMUA NA KUFANYA KWA MSIMAMO BILA KUACHA.
Ukisimamia hilo, mafanikio kwako ni swala la muda tu.

Rafiki, hebu amua kuwa hivyo ambavyo wengi hawataki kuwa ili uweze kupata mafanikio makubwa unayoyataka.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe