3525; Hujamaanisha Kama Huwezi Kurahisisha Hivi.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Mafanikio makubwa, kila mtu anayatamani.

Lakini kutamani pekee hakutoshi kumpa mtu mafanikio makubwa anayoyataka.

Ni lazima amaanishe hasa.

Na kumaanisha kwamba unayataka mafanikio na upo tayari kuyapambania, lazima uweze kurahisisha hivi.

Moja ni lazima uweze kueleza kwa urahisi ni matokeo gani unayotaka kupata.
Yaani ni nini hasa unachotaka?
Usieleze vitu vya jumla jumla kama; nataka fedha nyingi.
Fedha nyingi ndiyo nini?
Eleza hasa unachotaka, kama ni fedha, eleza ni kiasi gani.

Mbili ni lazima ueleze kwa nini unataka unachotaka. Kwa nini umechagua hivyo na siyo vinginevyo?
Kwa nini uwe tayari kupambana kupata unachotaka?
Kama huwezi kueleza kwa nini unataka unachotaka, hicho siyo chako, umeiga tu kwa wengine.
Na huwezi kupata kitu ambacho umeiga kwa wengine, lazima ndani yako uwe na sababu hasa ya kutaka kitu.

Tatu ni lazima ujue ni hatua zipi unazochukua ili kupata unachotaka.
Lazima ujue mambo hayatatokea yenyewe, ni mpaka yasababishwe.
Je wewe unasababishaje unachotaka?
Ni hatua zipi unachukua ili kupata unachotaka?
Kutaka upate kitu wakati haupo tayari kuchukua hatua, ni kujidanganya tu.

Rafiki, kwa lengo unalofanyia kazi sasa, hebu eleza kwa urahisi kwa ngazi hizo tatu, NINI unataka, KWA NINI unataka na VIPI unapata.
Huo ni mwongozo wa haraka utakaokupa chochote unachotaka.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe