3527; Tumia ulichonacho, kupata ambacho huna.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Huwa kuna usemi wa Kiswahili kwamba Mungu akikupa kilema, hakunyimi mwendo.
Ukweli ni kwamba kila mtu kuna vitu ambavyo amekosa ili kuweza kufika kule anakotaka kufika.
Hiyo ni hali ambayo ipo kwa kila mtu.
Lakini uzuri ni kwamba pamoja na kukosa vitu ambavyo tunavitaka sana, huwa kuna vingine tunavyokuwa navyo, tena kwa wingi.
Ni hivyo tunavyokuwa navyo ndiyo tunaweza kuvitumia kupata vile ambavyo hatuna.
Hivyo ndivyo ilivyo mara zote.
Unaweza kupata chochote unachotaka, lakini ni kama tu utatumia vizuri vile ulivyonavyo sasa.
Unapokuwa unaanza biashara, au biashara yako ikiwa chini, kila kitu kinakuwa kigumu na hakuna matokeo.
Unakuwa huna ujuzi sahihi unaohitaji, huna fedha kwa ajili ya mtaji na kuna watu sahihi ambao wanaweza kukusaidia.
Kwa kifupi ni unakuwa huna maisha.
Lakini kuna kitu kimoja unachokuwa nacho kwa wingi, MUDA.
Unakuwa na muda mwingi ambao ukiweza kuutumia vizuri, utakupa hivyo vingine vyote. Muda utakupa maisha.
Unaweza kutumia muda wako kujenga ujuzi sahihi unaohitaji kuwa nao ili biashara ipige hatua. Hakuna cha kukukwamisha kwenye hilo, maana ujuzi unapatikana bure kabisa, ni wewe tu.
Kadiri unavyojenga ujuzi wako, ndivyo kipato chako pia kinavyoongezeka. Hapo unaanza kupata pesa. Na ukiendelea kujenga ujuzi mkubwa zaidi unakuza kipato chako zaidi.
Ukiwa na pesa unaweza kuwavutia watu sahihi kuja kwako, ambao watakusaidia kwenye mengi unayohitaji.
Rafiki, kama unakosa vyote kwenye mafanikio, anza kutumia muda wako vizuri, kujenga ujuzi utakaokulipa sana kisha utaweza kujenga koneksheni sahihi.
Itashangaza sana kama utakuwa huna vyote unavyotaka na huna muda pia.
Hapo utakuwa umeamua kuwa na maisha duni milele.
Hata kama unakosa kila kitu, basi hakikisha muda wako huukosi, maana huo ndiyo mkombozi sahihi kwako.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe