Habari njema wauzaji bora kuwahi kutokea.

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya CHUO CHA MAUZO, yenye lengo la kutujenga kuwa wauzaji bora na kufanya mauzo makubwa.

Mkakati wetu mkuu kwenye CHUO CHA MAUZO ni kutengeneza wateja tarajiwa na kuwafuatilia wateja mara zote. Kwa kufanya hayo mawili, kufanya mauzo makubwa inakuwa ni matokeo ya uhakika.

Zawadi ni moja ya njia ambazo biashara zinaweza kutumia kuwafikia wateja wengi na kuwashawishi kununua kile kinachouzwa. Hiyo ni kwa sababu watu huwa wanapenda zawadi na huwa wanalipa fadhila kwenye kile wanachopokea.

Zawadi zinapokuwa ni za vitu ambavyo mtu anakaa navyo kwa muda mrefu na zikawa na nembo na jina la biashara, huwa zinawafanya watu kuendelea kukumbuka kuhusu biashara na kushawishika kununua.

Ipo njia ya kuwafanya watu wazithamini zaidi zawadi wanazopokea na kukaa nazo kwa muda mrefu. Kwa njia hiyo, wale wanaopata zawadi wanapata msukumo wa kuwaonyesha wengine na hilo kusaidia kwenye kuwafikia watu wengi zaidi.

Njia hiyo ya kuwafanya wateja wathamini zaidi zawadi ni kuweka majina ya wateja kwenye zawadi ambazo wanapokea. Jina la mtu ndiyo sauti ambayo mtu anapenda sana kuisikia, ndiyo kitu kinachoshika umakini wa kila mtu. Pale mtu anapopewa zawadi yenye jina lake, ataitunza na kuwaonyesha wengine kama sehemu ya kuonyesha kwamba anatambuliwa na kuheshimiwa.

Ni kupitia wateja kuwaonyesha wengine zawadi zenye majina yao ndiyo jina la biashara iliyotoa zawadi hizo husambaa kwa wengi zaidi. Wale wanaoona wenzao wakiwa na zawadi zenye majina yao nao huvutiwa kuja kununua kwenye biashara ili pia wapate zawadi zenye majina yao.

Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza jinsi ya kutekeleza hilo kwa mafanikio makubwa. Karibu ujifunze.

AINA ZA ZAWADI ZENYE MAJINA YA WATEJA.

Zipo aina mbalimbali za zawadi zenye majina ya wateja zinazoweza kutumika kuwafikia wateja wengi zaidi.

Baadhi ya zawadi zinazoweza kutumika kwa ushawishi mkubwa ni kama ifuatavyo.

1. Mavazi ya michezo.

Mavazi ya michezo huwa watu wanapenda kuyavaa, hasa pale yanapokuwa ya timu wanazoshabikia na kuwa na majina yao. Tisheti za michezo za timu ambayo mteja anashabikia na ikawa na jina lake mgongoni ni kitu ambacho atajivunia kuvaa mara nyingi.

2. Vyombo vya kunywea.

Vyombo ambavyo watu wanatumia kunywa vitu mbalimbali vikiwa na majina ya watu vinawashawishi kutumia mara kwa mara na muda mrefu. Vyombo hivyo ni kama vikombe vya kunywea chai au kahawa na glasi za kunywea vinywaji moto au baridi. Mtu hujisikia vizuri pale anapoona jina lake kwenye chombo anachotumia kila siku.

3. Vishika funguo.

Vifaa vinavyotumika kushika na kutunza funguo huwa vinatumiwa na watu kwa muda mrefu. Pale vifaa hivyo vinapokuwa na jina la mtu, anavithamini zaidi kwa sababu anajua hata akipoteza funguo zake, watu watajua ni za nani na kuweza kumpatia. Watu watatunza kwa umakini sana vifaa vya kushika funguo vyenye majina yao.

4. Kalamu na vitabu.

Kalamu na vitabu ambavyo watu wanatumia kuandika mambo yao mbalimbali huwa wanakuwa navyo muda mwingi. Pale kalamu na vitabu hivyo vinapokuwa na majina ya watu, wanavithamini na kuvitunza zaidi. Watapenda kuvitumia kwenye maeneo ambayo wengine wanaweza kuona ili kuonekana wao ni muhimu.

5. Vyeti na Tuzo.

Watu wanapopata vyeti na tuzo za aina mbalimbali, huwa wanazitunza kama sehemu ya kumbukumbu za wao kuthaminiwa. Vyeti na tuzo hizo huwa na majina ya watu na kile ambacho wameweza kufanikisha. Watu huwa wanahakikisha wanaweka vyeti na tuzo hizo maeneo ambayo wengine wanaweza kuona, kwa sababu inawafanya wajisikie vizuri.

Zawadi zenye majina ya watu zinazoweza kutumika ni nyingi, hapa tumeangalia chache ambazo zina ushawishi mkubwa. Lakini kila kitu ambacho mtu anaweza kukitumia kwa muda mrefu au mfupi kinaweza kuwekwa jina lake na hiyo ikampa msukumo wa kuwaonyesha wengine wengi zawadi hiyo. Kupitia kuwaonyesha wengi ndivyo jina la biashara yako linasambaa na kuwafikia wengi.

SOMA; Tumia Sikukuu Na Siku Maalumu Kufikia Wateja Wengi Zaidi.

MAMBO YA KUZINGATIA KWENYE KUTUMIA ZAWADI ZENYE MAJINA.

Ili kutumia zawadi zenye majina kuwafikia watu wengi zaidi na kutengeneza wateja tarajiwa, mambo yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa;

1. Zawadi iendane na biashara.

Tumeona kuna zawadi mbalimbali ambazo biashara inaweza kutoa. Ili zawadi iwe na nguvu, inapaswa kuendana na kile ambacho biashara inafanya. Kama biashara inafanya mambo yanayoendana na michezo, zawadi za mavazi ya michezo zinakuwa na nguvu zaidi. Kwa maneno mengine, zawadi ambayo mteja anapewa iwe inaendana na kile ambacho biashara inafanya.

2. Zawadi iwe ni kitu ambacho mteja anajali.

Zawadi pia inapaswa kuwa kitu ambacho kina maana na matumizi kwa mteja. Kwa sababu lengo la zawadi yenye majina siyo tu mteja apokee, bali pia atumie kwa namna ambayo wengine wataona. Kwa zawadi kuwa kitu ambacho mteja ana matumizi nacho, inakuwa na nguvu kwenye kuwafikia wengine na kuwashawishi kuwa wateja pia.

3. Zawadi iwe inayodumu muda mrefu na kutumika kirahisi.

Kuna zawadi ambazo mtu anatumia mara moja na kuwa zimeisha, hasa vitu vya kula, hizo zinaweza kuwekewa majina, lakini nguvu yake haitakuwa kubwa kama kwa zawadi zinazodumu muda mrefu. Toa zawadi ambazo mtu anakaa nazo kwa muda mrefu na kutumia kwa urahisi ili wengi waweze kumwona mtu akiwa na zawadi hiyo na kushawishika kujua zaidi.

4. Zawadi iwe na nembo, jina na mawasiliano ya biashara.

Zawadi kuwa na jina la mteja peke yake haitoshi, lazima pia iwe na kitu ambacho kinaitambulisha biashara. Hivyo zawadi inapaswa kuwa na nembo, jina na ikiwezekana mawasiliano ya biashara. Hiyo inawafanya wengine wanaoiona zawadi wajue imetoka wapi na kushawishika kuchukua hatua ili nao waweze kupata zawadi kama hiyo.

5. Zawadi iwe ambayo biashara inaweza kumudu.

Zawadi ambazo biashara inatoa kwa wateja wake zinapaswa kuwa na tija. Yaani gharama zinazotumika kwenye kutoa zawadi ziwe ni ambazo biashara inaweza kuzimudu kulingana na faida inayopatikana na wateja wanaoweza kufikiwa. Biashara lazima iangalie zawadi ambayo itakuwa na nguvu ya kuwafikia wateja wengi zaidi kwa gharama ambazo biashara inaweza kumudu. Hilo litaepusha biashara kuingia gharama kubwa na kupata hasara kwenye zoezi la kutoa zawadi.

Watu huwa wanapenda na kuthamini zawadi wanazopewa na pale zawadi inapokuwa na majina yao, wanatunza na kuonyesha kwa watu wengi zaidi. Pale zawadi inapoonyeshwa kwa watu wengi, inawashawishi na wao kuchukua hatua ili kupata zawadi kama hiyo. Kutoa zawadi zenye majina ya wateja ni njia nzuri kwa biashara kuweza kuwafikia watu wengi zaidi na kuwashawishi kuwa wateja kwa zawadi wanazokwenda kupata. Andaa mkakati wa kutoa zawadi zenye majina kwa wateja ili kushawishi wengi kuwa wateja.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.