3528; Ni mapambano yako peke yako.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Unapokuwa unaanzia chini kabisa, yaani ndiyo unayaanza mapambano, kila mtu atakuwa anakushangilia kwa hayo matamanio yako.

Lakini siyo wote wanaokushangilia wanataka ufanikiwe au ukifanikiwa watafurahi.

Wengi wa wanaokushangilia wanaamini kabisa hutaweza kupata makubwa unayotaka.
Hivyo wanataka tu waonekane walikuunga mkono, japo kwa ndani hawakuwa na wewe.

Hutazijua sura halisi za watu mpaka pale utakapoanza kupiga hatua kubwa na zinazowazidi wao.
Hapo sasa ndiyo wanaonyesha makucha yao, kwa sababu wanakuwa hawawezi tena kuficha.

Kama unategemea kukubalika au kuungwa mkono na wengi kwenye safari yako ya mafanikio, utakwama.

Kama unataka mafanikio makubwa kwenye maisha yako, usijali wengine wanafikiriaje kuhusu wewe.

Jua siyo watu wote watakupenda, wengi watakuchukia pale unapofanya vizuri kuliko wao.

Wivu ni mwingi kuliko wengi wanavyofikiri. Wengi wanaokupongeza na kuonekana kukuunga mkono, wanakuwa na wivu ndani yao unapofanya vizuri kuliko wao.

Ni muhimu kujikumbusha kwenye safari ya mafanikio makubwa, uko peke yako. Jiamini kwamba utaweza na pambania kile unachotaka bila kujali wengine wanasema au kufanya nini.

Kikubwa zaidi, watafute watu ambao wanataka kweli wewe ufanikiwe.
Ambao wanashangilia na kufurahia kweli pale unapopiga hatua zaidi.
Watu hao wapo, japo ni wachache sana.

Kabla hujawapata na kuamini kabisa, ni vyema kujichukulia unapambana peke yako. Itakuepusha kuangushwa na kuumizwa na wengine.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe