3529; Kiungo cha kubadilisha kama unataka mafanikio makubwa.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Moja ya sifa zetu binadamu ni kutokuridhika na maumbile ambayo tumezaliwa nayo.
Hii hali ipo kwa kila mtu na kulingana na uwezo wa mtu, zimekuwa zinafanyika jitihada mbalimbali za kubadili maumbile hayo.
Ndiyo maana watu wanaweka nywele zao dawa ili zionekane vizuri, au kuvaa nywele za bandia kabisa.
Wengine wanabadili rangi ya nywele, ngozi, kucha na vitu vingine vinavyoshangia mwonekano wao.
Na kama hiyo haitoshi, watu wameenda mbali zaidi na kubadili sura, vifua, tumbo na matako ili kuwa na mwonekano wa aina fulani.
Mabadiliko yote hayo ambayo watu wanafanya kwenye miili yao, huwa yanawagharimu fedha, muda na rasilimali nyingine.
Lakini marejesho ambayo watu wanayapata kwa uwekezaji huo wanaofanya huwa siyo makubwa sana.
Wanaishia kujisikia vizuri na kusifiwa na wengine.
Kuna kiungo kimoja ambacho mtu akiweza kukibadilisha, atapata marejesho makubwa sana, maana hakuna gharama yoyote anayokuwa ameingia.
Kiungo hicho ni ubongo wako ambao ndiyo unakujenga namna unavyofikiri na kufanya mambo yako.
Namna ya kuubadili ubongo wako ili iwe na manufaa kwako kifikra, yaani kuongeza akili yako ni kuwa na shauku kubwa.
Kuwa na shauku ni sawa na kuongeza akili yako kwa alama 25 (IQ points).
Yaani kuwa na shauku kubwa ni sawa na kufanyiwa operesheni ya ubongo na kuongezewa akili.
Habari njema ni kwamba huhitaji kulipa gharama yoyote kwenye hilo zoezi.
Ni wewe tu uamue kuwa na shauku kwenye kila jambo unalofanya.
Watu wenye shauku huwa na nguvu inayowasukuma kufanya makubwa kitu kinachowapa fursa nzuri za kufanikiwa zaidi.
Kwa zama hizi ambazo ushindani umekuwa mwingi kwenye kila jambo, chagua kuwa mtu mwenye shauku kubwa kwenye mambo yako yote.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe