3532; Kitakachokuinua Tena.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Kwenye safari yako ya kupata mafanikio makubwa kwenye maisha, vikwazo, changamoto na kuanguka ni sehemu ya safari hiyo.

Hakuna namna utataka makubwa halafu usikutane na vikwazo vinavyokuangusha kabisa.

Kinachotokea baada ya kuanguka ndiyo kinaamua hatima ya safari yako ya mafanikio.

Kwa walio wengi, ambao ndiyo huwa wanashindwa, huo huwa ndiyo mwisho wa safari yao.
Wakishaanguka wanaona ndoto zao haziwezekani tena.

Wapo wanaobaki hapo walipoanguka na wapo wanaoenda kuanza vitu vingine vipya kabisa.
Lolote kati ya hayo halina msaada kwa mtu kufanikiwa.

Wachache sana, ambao ndiyo wanaopata mafanikio makubwa huwa wanainuka na kuendelea na safari baada ya kuanguka.
Hata waanguke mara nyingi kiasi gani, bado watainuka na kuendelea na safari.

Unaweza kujiuliza ni nini kinawasukuma hao wachache kuinuka na kuendelea na safari.

Jibu ni moja, njaa kali sana ya mafanikio isiyoshibishwa na chochote.

Kwenye maisha, kiumbe yeyote hai, akiwa na njaa huwa tayari kufanya kitu chochote kile ili kupata chakula.

Hata kwenye utawala wa nchi, wananchi huwa tayari kuondoa utawala pale wanapokuwa na njaa hasa.

Maana mtu anapokuwa na njaa, anakuwa hana cha kupoteza.
Anaona kama hawezi kupata chakula, maisha yana maana gani nyingine?

Hivyo ukiweza kuwa na njaa kali sana ya mafanikio, njaa isiyoshiba hata pale unapopiga hatua fulani, hakuna kitakachokuzuia kufanikiwa.

Njaa hiyo kali ndiyo itakayokusukuma kuinuka tena bila kujali umeanguka mara ngapi.
Ndiyo itakufanya uendelee kupambana bila kuchoka.

Unaweza kujijengea njaa hiyo ya mafanikio makubwa kwa kuwa na ndoto kubwa ambazo unaamini, bila ya shaka yoyote kwamba utazifikia.

Jione kabisa ukiwa tayari umeshatimiza ndoto kubwa ulizonazo na fanyia kazi kuzifikia kwa uhakika.

Nenda hivyo mpaka ufikie ndoto zako na ukishazifikia, zikuze zaidi.
Utaenda kwa mpango huo kwa siku zote za uhai wako hapa duniani.
Na utaweza kufanya makubwa sana.

Usikubali kuishi maisha madogo ya kukwamishwa na vikwazo na changamoto.
Ishi maisha makubwa ya kupata chochote unachotaka bila ya kuzuiwa na chochote.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe