3533; Usirudie Mara Mbili.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Kuna mafunzo kuhusu mafanikio, ambayo mtu ukiyaendea kichwa kichwa yatakupoteza sana.

Na hilo ndiyo limekuwa linawakwamisha na kuwapoteza wengi, kupokea maarifa nusu nusu na kukimbilia kuyafanyia kazi bila kuyaelewa.

Matokeo yake ni watu kupoteza zaidi kuliko kunufaika.

Huwa kuna kauli maarufu kwamba kama hukosei basi hakuna makubwa unayojaribu kufanya.

Baadhi ya waliofanikiwa huwa wanasema wazi kwamba hawawaamini watu ambao hawajawahi kukosea.
Maana hao ni watu wanaocheza salama sana.

Wengi kwa kusikia hivyo, wanakimbilia kukosea ili waonekane wanapambania makubwa.
Na wanakosea kweli kweli, kitu kinachowadidimiza badala ya kuwainua.

Maarifa yaliyokamilika kwenye kukosea ni haya; ILI UFANIKIWE UNAPASWA KUFANYA MAKOSA MENGI, LAKINI USIRUDIE KOSA MOJA MARA MBILI.

Hiyo sehemu ya pili ndiyo muhimu zaidi lakini ambayo imekuwa inapuuzwa na wengi.

Kosea ndiyo, lakini usirudie kosa moja mara mbili.
Lengo la kukosea ni kujifunza, hivyo ukishajifunza unapaswa kufanya kwa ubora zaidi.

Ukirudia kosa moja mara mbili maana yake hujifunzi.
Na kama hujifunzi huwezi kupata mafanikio makubwa unayoyataka.

Jaribu mambo mapya na makubwa kuliko ulivyozoea. Utakosea, ila jifunze na usirudie tena kukosea kwa namna ile ile.
Ukishakosea pata somo na fanya kwa ubora zaidi.

Ukishaeleza dhana hiyo ya kutokukosea mara mbili, ndipo sasa unaweza kufanyia kazi ushauri wa Watson aliyesema; Kuongeza kasi yako ya mafanikio, ongeza kasi yako ya kushindwa.”

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe