3534; Watu hawabadiliki.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye maisha na hii safari yetu ya mafanikio, tunawahitaji sana watu.
Tunawahitaji watu kuanzia kwenye maisha yetu binafsi na kwenye shughuli mbalimbali tunazofanya.
Hilo linatutaka tuwe wazuri sana kwenye mahusiano yetu na watu wengine.
Kujenga na kutunza mahusiano na watu imekuwa ni kazi kubwa na yenye changamoto zake.
Na hiyo ni kwa sababu watu wamekuwa hawaeleweki.
Unaweza kuwategemea wawe kwa namna fulani, ila wao wakawa kwa namna nyingine tofauti kabisa.
Hilo limekuwa linapelekea tuone watu wanabadilika, kwa sababu mwanzo walikuwa kwa namna fulani, ila sasa wapo kwa namna nyingine.
Lakini ukweli ni kwamba watu huwa hawabadiliki.
Badala yake mahitaji yao ndiyo huwa yanabadilika.
Na mahitaji yao yakibadilika, huwa wanaendana nayo.
Hiyo ni kusema kwamba watu siyo waaminifu kwako, bali kwa mahitaji yao wenyewe.
Kinachowasukuma watu kuwa vile walivyo, ni mahitaji ambayo wanayo.
Na pale mahitaji hayo yanapowataka wewe uwepo kwenye maisha yao, wataonekana ni waaminifu kwako.
Lakini pale mahitaji yao yatakuwa hayakuhitaji tena, hawatakuwa tena waaminifu kwako.
Hilo linaweza kukuchanganya, kwa kushindwa kuelewa nini kimewabadili watu.
Lakini ukweli ni huo uliojifunza, watu hawabadiliki, bali wanafuata mahitaji yao.
Ufanye nini ili kukabiliana na hilo?
Ni kuwa wewe, kufanya yale yaliyo sahihi mara zote.
Hilo litawavuta wale walio sahihi kwako katika kipindi hicho cha maisha yao.
Lakini haimaanishi watakuwepo milele, kwani vipindi vya maisha yao vinapobadilika na wakawa hawakuhitaji tena, hawataendelea kuwepo.
Kulijua hili kunakupa utulivu mkubwa sana na kukufanya uache kukimbizana na kujaribu kumridhisha kila mtu.
Mtu pekee anayeweza kuwa mwaminifu kwako wakati wote ni wewe mwenyewe.
Na hilo ni kama utachagua kuyaishi maisha yako na kuacha kuhangaika kumridhisha kila mtu.
Usiwalalamikie tena watu kwamba wamebadilika na kuacha kuwa waaminifu kwako.
Jua mahitaji yao yamebadilika na hawakuhitaji tena kama ilivyokuwa awali.
Hivyo ndivyo maisha yalivyo, ukiyaelewa hakuna litakalokusumbua katika kuyaishi.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe