Habari njema wauzaji bora kuwahi kutokea.
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya CHUO CHA MAUZO, yenye lengo la kutujenga kuwa wauzaji bora na kufanya mauzo makubwa.
Mkakati wetu mkuu kwenye CHUO CHA MAUZO ni kutengeneza wateja tarajiwa na kuwafuatilia wateja mara zote. Kwa kufanya hayo mawili, kufanya mauzo makubwa inakuwa ni matokeo ya uhakika.
Kutengeneza wateja wapya tarajiwa ni hatua muhimu sana kwenye kukuza mauzo, kwa sababu ndiyo inaleta wateja wapya kwenye biashara. Na ukuaji wa biashara yoyote ile unategemea wateja wapya ambao inawafikia na kuwashawishi kununua.
Zoezi zima la kufikia wateja wapya wengi zaidi huwa lina gharama zake. Kunahitajika rasilimali mbalimbali, ikiwepo fedha, ujuzi, teknolojia na watu ili kuweza kuwafikia wateja tarajiwa sahihi kwa biashara.
Mara nyingi biashara moja inaweza ikashindwa kumudu kuwa na rasilimali zote zinazohitajika ili kuweza kufikia wateja wengi zaidi kama ambavyo inahitaji. Na hapo ndipo ushirikiano wa kibiashara unapoweza kuwa na manufaa ya kuiwezesha biashara kutumia rasilimali za biashara nyingine kufikia wateja wengi zaidi.
Ushirikiano wa kibiashara kwenye kutengeneza wateja wapya tarajiwa ni pale biashara zinapoamua kushirikiana kwenye kutumia rasilimali ambazo zinazo ili kuweza kufikia wateja wengi zaidi kwa manufaa ya kila biashara. Kwa kushirikiana kwenye kutumia rasilimali ambazo biashara tayari zinazo, matokeo huwa ni makubwa kwa biashara zote kuliko kila biashara kujitegemea yenyewe.

Kushirikiana kibiashara kuwafikia wateja wengi zaidi inatumia vizuri dhana ya umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Kwa kushirikiana pamoja kwenye kuwafikia wateja, kila biashara inapata matokeo makubwa kuliko ingefanya peke yake.
FAIDA ZA USHIRIKIANO WA KIBIASHARA KUWAFIKIA WATEJA WENGI.
Ushirikiano wa kibiashara kwenye kuwafikia wateja wengi una faida nyingi kwa kila biashara inayoshiriki. Baadhi ya faida hizo ni kama ifuatavyo;
1. Kufikia Hadhira Mpya.
Biashara zinaposhirikiana zinapata fursa ya kufikia hadhira mpya, ambayo kila biashara isingeweza kufikia peke yake. Hiyo inaongeza fursa za kutengeneza wateja wapya tarajiwa kutoka kwenye hadhira hizo mpya.
2. Kupunguza Gharama.
Ushirikiano wa kibiashara kufikia wateja inapunguza gharama za kufikia na kutengeneza wateja kwa kila biashara. Hiyo ni kwa sababu kila biashara inatumia rasilimali za biashara nyingine kufikia watu wengi. Na hata kwa baadhi ya gharama, mfano za matangazo, zinapochangiwa na biashara zaidi ya moja zinapungua kwa kila biashara.
3. Kuaminika Zaidi.
Biashara inapoenda kwenye soko jipya, inakuwa haiaminiki kwa sababu haijulikani. Lakini inaposhirikiana na biashara nyingine ambayo tayari inaaminika kwenye soko husika, kunafanya biashara iliyokuwa mpya nayo kuaminika. Pia biashara zinaposhirikiana zinaaminika zaidi kuliko kila moja ikifanya kivyake.
4. Kunufaika Na Rasilimali Mpya.
Ushirikiano wa kibiashara unatoa fursa kwa biashara kunufaika na rasilimali mpya ambazo haikuwa nazo. Rasilimali hizo zinaweza kuwa teknolojia mpya, ujuzi wa kipekee, njia za kufikia wateja na mifumo ya kuwafuatilia wateja. Kwa kutumia rasilimali hizo mpya, biashara inanufaika sana.
5. Kuweza Kufanya Masoko Ya Pamoja.
Ushirikiano wa kibiashara unatoa fursa ya kufanya masoko ya pamoja, kama kulipia na kutumia tangazo moja, kubadilishana wateja na hata kutengeneza kifurushi kimoja ambacho kinampa mteja thamani kubwa zaidi. Mfano mzuri hapa ni migahawa ya vyakula vya haraka (McDonalds) na kampuni za vinywaji baridi (CocaCola).
Biashara zinaposhirikiana pamoja kuwafikia wateja wengi zaidi, manufaa kwa kila biashara yanakuwa makubwa huku gharama zikiwa ndogo.
SOMA; Tumia Orodha Mbalimbali Kufikia Wateja Wengi Zaidi.
AINA ZA USHIRIKIANO WA KIBIASHARA KUWAFIKIA WATEJA WENGI ZAIDI.
Pamoja na kwamba biashara zinashirikiana pamoja kuwafikia wateja wengi zaidi, kuna aina mbalimbali za namna ushirikiano huo unaweza kufanyika na kuwa na manufaa kwa biashara zote. Hapa kuna baadhi ya aina za ushirikiano huo;
1. Ushirikiano Wa Kimkakati.
Hapa biashara zinashirikiana kimkakati kuleta matokeo makubwa kwa kila biashara. Hii inahusisha kushirikiana kwenye rasilimali na ujuzi wa kuwafikia wateja. Pia inahusisha kufanya masoko ya pamoja kitu ambacho kinawezesha kila biashara kufikia wateja wengi kwa gharama nafuu.
2. Ushirikiano Wa Kutangaziana.
Huu ni ushirikiano ambapo biashara zinatangaziana, yaani biashara moja inatangaza biashara nyingine kwa wateja wake na pale mteja anaponunua kunakuwa na kamisheni inayolipwa kwa biashara iliyotangaza. Ushirikiano huu unawezesha biashara kutumia imani ambayo tayari biashara nyingine inayo kwa wateja wake na wakashawishika kununua.
3. Ushirikiano Wa Ubia.
Hapa biashara zinakuwa na ubia kwenye kuwafikia wateja wengi zaidi. Ubia huu unahusisha kufanya masoko kwa pamoja, mfano kufanya tangazo moja na hivyo kugawana gharama. Kila biashara inafikia wateja wengi bila kuingia gharama. Ubia pia unaweza kufikia ngazi ya biashara tofauti kuja na bidhaa au huduma moja ambayo inauzwa na wote kitu kinachopelekea ifanye vizuri zaidi.
4. Kubadilishana Orodha.
Huu ni ushirikiano ambapo biashara zinabadilishana orodha za wateja wao kitu kinachorahisisha kuwafikia wateja wengi wapya. Pale biashara zinapokuwa na wateja wanaofanana sifa lakini hazina ushindani wa moja kwa moja, hii ni njia nzuri ya kupata wateja tarajiwa ambao ni rahisi kuwageuza kuwa kamili.
5. Ushirikiano Wa Rufaa.
Hapa biashara zinakuwa na makubaliano ya kupeana rufaa ambapo kila biashara inawashawishi wateja wake kwenda kununua kwenye biashara ambayo wanashirikiana. Pale mteja anapokuwa na uhitaji wa kitu ambacho biashara haiuzi, wakishawishiwa na biashara wanayoiamini wapi sahihi kwenda kununua, huwa wanaamini zaidi.
Aina za ushirikiano wa kufikia wateja wengi ni nyingi, biahsara zinazotaka kushirikiana kwenye eneo hilo zinaweza kuangalia aina ambayo ina manufaa makubwa kwa wote wanaoshiriki.
SOMA; Tumia Zawadi Zenye Majina Kufikia Wateja Wengi Zaidi.
MIKAKATI YA KUPATA WASHIRIKA SAHIHI KWENYE KUFIKIA WATEJA WENGI ZAIDI.
Kupata washirika sahihi ni hatua muhimu kwenye kunufaika na ushirikiano wa kibiashara wa kufikia wateja wengi zaidi. Ushirikiano usipokuwa sahihi, unaishia kudhuru biashara zote zinazoshiriki. Ili kuhakikisha unapata washirika sahihi, zingatia yafuatayo;
1. Weka Malengo Yako Ya Kufikia Wateja Wengi Zaidi.
Anza na malengo uliyonayo kwenye kuwafikia wateja wengi zaidi ndiyo uweze kujua ni washirika wa aina gani unaowahitaji ili kuweza kuwafikia wateja hao. Malengo unayoweka yanahusisha ni aina gani ya wateja unaotaka kuwafikia, kiasi gani, gharama unazoweza kuingia na muda ulionao kwenye kukamilisha hilo.
2. Tafiti Washirika Sahihi Kushirikiana Nao.
Ukishakuwa na malengo, kinachofuata ni kujua washirika wapi sahihi watakaokuwezesha kufikia malengo hayo. Pitia biashara nyingi kuweza kuona zipi ambazo unaweza kushirikiana nazo kwa manufaa.
3. Angalia Biashara Zinazoendana.
Hatua muhimu sana kwenye kuchagua washirika wa kibiashara kwenye kufikia wateja ni kuhakikisha hakuna ushindani wa moja kwa moja. Huo huwa hauishii vizuri, kwa sababu kila biashara inatafuta njia ya kupiku wengine sokoni. Chagua biashara ambazo zinalenga wateja wenye sifa sawa, lakini hakuna ushindani wa moja kwa moja. Kwa njia hii kunakuwa hakuna mgongano wa kimaslahi, badala yake wote mnanufaika.
4. Tathmini Ushirikiano Utakavyokwenda.
Baada ya kufanya utafiti na kupata washirika sahihi ambao unaweza kwenda nao, tathmini jinsi ushirikiano huo utakwenda na manufaa ambayo kila upande utapata. Jua ni aina gani ya ushirikiano utafanyika, wajibu wa kila upande unakuwa upi na manufaa ambayo kila upande unakwenda kupata ni yapi. Pale tathmini hiyo inapoonyesha kila upande unaweza kumudu na kunufaika, ndiyo ushirikiano unaweza kuendelea.
5. Omba Rufaa.
Katika kupata washirika sahihi, omba rufaa kwenye biashara ambazo zipo sokoni au kutoka kwa vinara wa soko. Kwa kutumia rufaa utapata washirika ambao ni sahihi, kwa sababu watu wanaoaminika wanakuwa wamewapendekeza. Hiyo itakupunguzia wewe kufanya makosa kwa kutokuwa na uelewa sahihi wa wale unaotaka kushirikiana nao.
Ni muhimu kupanga na kuzingatia mambo ya msingi kwenye kuchagua biashara sahihi za kushirikiana nazo kwenye kuwafikia wateja wengi zaidi.
SOMA; Tumia Mtandao Wa Intaneti Kufikia Wateja Wengi Zaidi.
MAMBO MUHIMU KUZINGATIA KWENYE USHIRIKIANO WA KIBIASHARA WA KUFIKIA WATEJA WENGI.
Ushirikiano wa kibiashara kwenye kuwafikia wateja wengi ni kitu ambacho kinaweza kuwa na manufaa makubwa kwa wote wanaoshiriki. Lakini pia ni eneo linaloweza kuibua changamoto ambazo zinaweza kukwamisha zaidi kuliko kusaidia. Ili kuhakikisha changamoto haziibuki na kukwamisha ushirikiano, mambo yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa;
1. Ushirikiano Uelezewe Kwa Usahihi.
Kabla ya kuingia kwenye ushirikiano wa kibiashara ili kuwafikia wateja wengi, lazima ushirikiano huo uweze kuelezewa kwa usahihi. Lazima kila upande ujue ushirikiano ni wa aina gani, wajibu wa kila upande ni upi na manufaa yanayotegemewa ni yapi. Ni muhimu sana kila anayeingia kwenye ushirikiano huo awe na matarajio sahihi.
2. Mawasiliano Yanapaswa Kuwa Ya Mara Kwa Mara.
Kwenye ushirikiano wa aina yoyote ile, mawasiliano ni muhimu sana kuhakikisha wote mko upande mmoja. Hivyo pia ndivyo inavyopaswa kuwa kwenye ushirikiano wa kibiashara, pande zote zinapaswa kuwa na mawasiliano ya mara kwa mara ili kutafua mambo wanayokabiliana nayo na kuweza kupiga hatua zaidi.
3. Kuwa Tayari Kubadilika.
Pamoja na mipango mikubwa na mizuri mnayokuwa mmeweka kwenye ushirikiano wa kibiashara, mnapaswa kuwa tayari kubadilika kulingana na matokeo yanayopatikana. Ndiyo maana mawasiliano ya mara kwa mara ni muhimu, ili kujadili hatua zinazopigwa na kuona jinsi ya kuboresha.
4. Boresha Uaminifu.
Kwenye ushirikiano wa aina yoyote ile, uaminifu ni nguzo muhimu, ambayo ikivunjwa ushirikiano hauwezi kuendelea. Kwenye ushirikiano wa kufikia wateja wengi, biashara zinashirikishana rasilimali zake mbalimbali, ni muhimu kila biashara kuwa na uaminifu mkubwa na kutokutumia vibaya rasilimali za biashara nyingine kujinufaisha zaidi huku wengine wakiumia. Kunapaswa kuwa na uwazi mkubwa kwenye mambo yote yanayofanyika kwenye ushirikiano uliopo.
5. Pima Mafanikio.
Kuna malengo ambayo yalikuwepo kabla ya kuingia kwenye ushirikiano wa kibiashara wa kufikia wateja wengi zaidi. Mara kwa mara mnapaswa kupima mafanikio na ukuaji unaopatikana kutokana na ushirikiano unaofanyika. Ni maendeleo hayo ndiyo yatakayoamua maboresho gani yanapaswa kufanywa kwenye ushirikiano ili kila upande kunufaika zaidi.
Kupata tu watu wa kushirikiana nao haitoshi kuleta manufaa, lazima kufanya ushirikiano kwa usahihi ili kila upande upate matokeo ambayo usingeweza kupata wenyewe.
Kwenye biashara na mafanikio kwa ujumla, ushirikiano sahihi huwa unaleta matokeo makubwa kuliko kila mtu kufanya peke yake. Kwenye kufikia wateja wengi zaidi, biashara inahitajika kutumia rasilimali nyingi, ambazo inakuwa haina. Kwa kushirikiana vizuri na biashara nyingine, zoezi la kufikia wateja wengi linafanikiwa kwa rasilimali na gharama ambazo kila biashara inaweza kumudu. Kila biashara inapaswa kutumia mkakati huu wa ushirikiano wa kibiashara ili ifikie wateja wengi kwa gharama nafuu.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.