3536; Kupendwa na Kuchukiwa.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Sisi kama binadamu, moja ya vitu tunavyopenda sana ni kupendwa na kukubalika na watu wengine.

Huwa tunatamani watu wote wanaotujua watupende na kutukubali.
Tunataka watusemee vizuri kwa yale tunayofanya ili taarifa zetu zifike kwa wengi zaidi.

Lakini hivyo sivyo uhalisia ulivyo.
Kwa sababu hakuna namna tunaweza kupendwa na kukubalika na watu wote.

Hata tuwe tunakazana kufanya mambo mazuri kiasi gani, kuna watu wataamua tu kutuchukia kwa yale tunayofanya.
Kwa sababu labda wao walitamani kufanya hivyo ila wakashindwa.

Hayupo mwenye uwezo wa kuwafanya watu wote wampende na kumkubali, hata angefanya nini.

Huwa kuna kauli kwamba hata ukiweza kutembea juu ya maji bila kuzama, kuna watu watasema unafanya hivyo kwa sababu hujui kuogelea.
Hebu fikiria hapo, umeweza kufanya jambo kubwa lisilowezekana kabisa, lakini kuna watu wataona ulichofanya si lolote na kuona umeshindwa ambalo kila mtu anaweza.

Mtu mmoja amewahi kusema; “Sijui njia ya uhakika ya mafanikio, ila najua njia ya uhakika ya kushindwa ni kutaka kumfurahisha kila mtu.”

Hiyo ni kauli nzito sana, ambayo imebeba hiki tunachojadili hapa.
Kama unataka kupendwa na kila mtu, ni kujipa uhakika kwamba hutafanikiwa.

Utakazana kufanya yale ambayo unaona yanakubalika na wengi na kuacha yale ambayo wengi hawayakubali.
Mwishowe unajikuta uko na watu ambao wanakupuuza tu, kwa sababu hakuna cha tofauti unachofanya.

Unapojaribu kuwafurahisha wengine, unaacha kuwa wewe halisi. Unaishia kuwa na maisha ya maigizo na watu wanakupuuza kwa sababu wanashindwa kukuamini.

Kama unataka mafanikio makubwa, ni lazima uamue kuwa wewe, yule ambaye ni halisi kabisa kwako.

Kwa kuwa wewe halisi na kuishi hivyo bila ya kujificha au kujaribu kuwafurahisha wengine, utaibua makundi mawili ya watu.

Kutakuwa na kundi la watu watakaokupenda sana kwa namna ulivyo. Wengi ni wanaokuwa wanatamani nao kuwa hivyo, ila wanashindwa. Wanapokuona wewe, wanaliona tumaini fulani.

Pia kutakuwa na kundi la watu watakaokuchukia sana kwa namna ulivyo. Wengi wanaokuchukia ni wale ambao walijaribu kuwa hivyo, ila wakashindwa.
Wanapokuona wewe unafanya na kuweza, wanachukia kwa nini wewe uweze wakati wao walishindwa.

Wengi huwa wanakazana kupunguza wanaowachukia wakiamini ndiyo watapata wanaowapenda zaidi.
Lakini matokeo yake huwa ni kuishia kupuuzwa zaidi.

Kama unataka upate wengi wanaokupenda na kukukubali, unapaswa kuwa na wengi wanaokuchukia na kukukosoa.

Pale wengi wanapokuchukia na kukukosoa, wengi zaidi wanajua kuhusu wewe. Na kadiri wengi wanavyojua kuhusu wewe, ndivyo wanavyochagua upande wa kuwa.
Kuna ambao nao watakuchukia, lakini kuna ambao watakupenda.

Kuchukiwa na kupingwa ni matangazo ya bure, ambayo yatakufikisha kwa watu wengi zaidi.
Kadiri unavyochukiwa, ndivyo pia unavyopendwa.

Hivyo rafiki, chagua kuwa wewe, halisi kwako kwa kufanya yale unayotaka kufanya.
Wale wanaokuchukia na kukukataa, hakikisha unawapa kila sababu ya kufanya hivyo ili waseme zaidi kuhusu wewe.

Kwa wao kusema zaidi kukuhusu, ndivyo unavyowafikia wengi na kuweza kuongeza wanaokupenda na kukukubali.

Najua inauma sana kuchukiwa na kukataliwa, lakini ndiyo njia pekee ya kupendwa na kukubaliwa.

Ni bora uchukiwe na kukataliwa na wengi, kuliko kupuuzwa kabisa.
Maana unapopuuzwa, hakuna anayekuongelea.
Ila ukichukiwa, unaongelewa zaidi na hilo kufanya wengi kujua kuhusu wewe.

Ni kwa namna gani unapochagua kuwa wewe, ambaye ni halisi kwako inapelekea watu kukuchukia na kukukataa?
Kuwa hivyo kwa makusudi kabisa ili uwatibue wengi watakaokuchukia na kukupinga lakini pia kukufikisha kwa wengi zaidi.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe