3542; Yarahisishe Maisha Yako.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Watu huwa wanalalamika kwamba maisha ni magumu.
Lakini cha kushangaza, huwa wanazidisha ugumu wa maisha yao kwa jinsi wanavyoyaendesha.
Na hilo ndiyo limekuwa linapelekea watu wengi kukwama na kushindwa kupata mafanikio makubwa wanayoyataka kwenye maisha yao.
Ni kweli maisha ni magumu, kwa sababu ya mambo mengi ambayo tunapaswa kupambana nayo ili tuweze kupata tunachotaka.
Lakini tunaweza kuyarahisisha maisha yetu kwa kufanya mambo ya msingi kabisa.
Moja ni kufanya kile ambacho unajiita.
Kama unajiita mwandishi, basi andika.
Unajiita mfanyabiashara, fanya biashara kweli.
Unajiita mjasiriamali, jasiriamalika.
Unajiita mchapa kazi, chapa kazi kweli kweli.
Orodhesha yote ambayo umekuwa unajiita au unataka wengine kukuita kisha yafanye.
Kitendo tu cha kufanya yale unayojiita, kitakusogeza karibu na kuwa mambo hayo.
Mbili ni kutimiza yote unayoahidi.
Maisha yanakuwa rahisi pale unaposema utafanya kitu, halafu unakifanya kweli.
Ni wewe mwenyewe umeahidi kufanya kitu, basi hakikisha unakifanya kweli.
Hiyo ndiyo namna pekee wengine wataweza kukuamini, pale unapokuwa mtu wa kutimiza neno lako.
Kama unaahidi mambo wewe mwenyewe, halafu huyatekelezi, unafikiri kwa nini watu waendelee kukuamini?
Kila unaloahidi, lifanye kama unavyoahidi bila kutoa sababu au visingizio.
Kuwa mtu wa kutunza ahadi zako kutafanya uaminike na kupata fursa nzuri zaidi.
Tatu ni kuifanya kazi kuwa rafiki yangu namba moja.
Kwenye kila jambo, egemea upande wa kuweka kazi zaidi.
Wakati wengine wanatafuta njia za kukwepa au kupunguza kazi, wewe tafuta njia ya kuongeza kazi.
Wakati watu wanatafuta kufanya kidogo lakini walipwe zaidi, wewe tafuta kufanya zaidi.
Jijengee sifa ya mtu anayependa na kuweka kazi kuliko wengine na hiyo itafanya wengi kuja kwako wanapokuwa na uhitaji wa kile unachofanya.
Nne ni kujua hujui na hivyo kuwa tayari kujifunza muda wote.
Kuna mengi sana hujui, hivyo utayari wako wa kujifunza utatarahisisha sana maisha yako.
Kuona tayari unajua kila kitu kutakukwamisha sana kwenye yale unayofanya.
Kila siku hakikisha unaimaliza ukiwa umejifunza vitu vipya ambavyo hukuwa unavijua.
Na ukishajifunza, weka kwenye matendo ili uweze kunufaika na hayo unayoyajua.
Tano ni kujua haijaisha mpaka imeisha.
Kama upo hai, jua lipo tumaini.
Haijalishi upo chini kiasi hani, haijalishi umekosea na kushindwa kiasi gani, una fursa ya kufanya vizuri zaidi.
Uhai ni zawadi kubwa sana, ambayo ukiweza kuitumia vizuri itakupa chochote unachotaka.
Shukuru kwa uhai ulionao na usilalamikie chochote. Badala yake chukua hatua sahihi ili kupata kile unachotaka.
Usikwamishe na chochote kile, wewe endelea kusonga mbele.
Rafiki, nini umekuwa unafanya na kupelekea maisha yako kuwa magumu zaidi?
Ni hatua gani unakwenda kuchukua kuyarahisisha maisha yako zaidi ya yalivyo sasa?
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe