3543; Kukimbiza na Kuvutia.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Jinsi unavyotumia muda wako inaathiri sana matokeo unayopata.
Msingi wa kwanza na muhimu sana kwenye mafanikio ni kuwekeza vizuri muda wako, kwenye vitu ambavyo vina tija kubwa.

Kwenye kuwekeza muda, kuna vitu ambavyo huwa tunavikimbilia. Hilo hupelekea vitu hivyo kuzidi kutukimbia. Unaishia kutumia muda mwingi kuvikimbiza vitu hivyo na bado huvipati.

Halafu kuna vitu ambavyo unavivutia, unavifanya vije kwako vyenyewe. Hapa unatengeneza mazingira ambayo yanafanya vitu vije kwako badala ya wewe kuvikimbilia.
Huo ndiyo uwekezaji sahihi wa muda, kwa sababu vinavyokuja huwa vina utulivu na thamani kuliko vile unavyokimbiza.

Tuangalie mfano wa kipepeo ili tuelewane vizuri.
Ukitumia muda wako kukimbiza kipepeo, kitakimbia kwenda mbali zaidi.
Ukikazana ukikamate ndiyo unazidi kukipoteza.

Ukitengeneza bustani yako vizuri, utavutia vipepeo wengi kuja.
Ukiwekeza muda wako kwenye kutengeneza bustani nzuri na ya kuvutia, viepepo wengi watakuja kwenye bustani hiyo wenyewe.
Hutahitaji kutumia nguvu kubwa kukimbizana na kumata vipepeo, badala yake watajileta wenyewe.

Tuangalie hili kwenye pande mbili; biashara na maisha.

Kwenye biashara na kazi, huwa inasisitizwa mtu kujenga mtandao mkubwa, kwa sababu ukubwa wa utajiri wa mtu unalingana na ukubwa wa mtandao wake.

Kujenga mtandao, mtu anaweza kukimbizana na wale anaotaka kujuana nao. Lakini huwa ni vigumu kuwapata.
Lakini kama mtu akimua kuwekeza muda wake kufanya mambo makubwa na tofauti, atajulikana na wale anaowalenga, ambayo watakuja kwake wao wenyewe.

Kwenye maisha binafsi, watu wamekuwa wanahangaika kukimbizana na mambo mengi ili kupata furaha.
Lakini kadiri wanavyoikimbiza furaha, ndivyo anavyozidi kuikosa.
Lakini kama mtu akiamua kuweka muda kufanya yale ambayo ana msukumo nayo ndani yake, atajisikia vizuri na kuwa na furaha.

Vitu vingi kwenye maisha tumekuwa tunavikosa kwa sababu ya kukimbizana navyo.
Njia sahihi ni kuvutia vitu kuja kwako kwa kujenga mazingira sahihi kwenye kila unachojihusisha nacho.

Rafiki, ni vitu gani umekuwa unakimbizana navyo sana lakini huvipati?
Unawezaje kuanza kuvivutia vitu hivyo ili vije kwako vyenyewe?

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe