Habari njema Matajiri Wawekezaji,

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya NGUVU YA BUKU, ambapo tunajifunza na kufanya uwekezaji kwa hatua ndogo ndogo na kujenga utajiri kwa uhakika.

Kauli mbiu yetu kwenye NGUVU YA BUKU, ambayo pia ndiyo imani yetu ni KILA MTU ANAWEZA KUWA TAJIRI. Hilo tuna uhakika nalo kwa sababu kwa fedha ndogo ndogo ambazo kila mtu anazipata, tukiziwekeza kwa muda mrefu kwa msimamo bila kuacha, tunaweza kujenga utajiri mkubwa.

Tabia za msingi ambazo watu tunazo, ambazo ndizo zinazojenga haiba zetu, huwa zina athiri maeneo mengi ya maisha yetu. Zinaathiri mawasiliano na ushirikiano wetu na wengine.

Lakini pia tabia hizo huwa zinaathiri uwekezaji tunaofanya na utajiri tunaojenga. Kwa sababu haiba ni kitu ambacho watu hatufundishwi, tumekuwa hatujui athari zake.

Hivyo kuna baadhi ya vitu tumekuwa tunafanya kwa mazoea, lakini athari zake ni kubwa.

Ili kufanya uwekezaji sahihi na kuwa na usimamizi mzuri wa utajiri tunaojenga, tunapaswa kujua haiba zetu na jinsi ya kuzitumia kwa usahihi.

Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza jinsi ya kuzijua haiba zetu na kuzitumia kwa usahihi kwenye uwekezaji. Somo la kujua haiba ni pana, hapa tutaangalia zile tabia za msingi, ambazo ni rahisi mtu kujua unaangukia wapi.

HAIBA KWA MFUMO WA DISC.

Kuna mifumo mingi ya kujua haiba za watu, lakini inapokuja kwenye kazi, biashara na fedha, mfumo wa DISC ndiyo umekuwa una ufanisi mzuri. Mfumo wa DISC unagawa watu kwenye makundi manne kulingana na tabia zao za msingi. Makundi hayo ni Dominance (Ushindani), Influence (Ushawishi), Steadness (Utulivu) na Compliance (Umakini).

Hivi ndivyo unavyoweza kuwekeza na kusimamia vyema utajiri wako kulingana na haiba yako ya DISC:

HAIBA YA USHINDANI/UTAWALA (DOMINANT);

Sifa;

1. Wanyoofu (Direct).

2. Wafanya maamuzi (Decisive).

3. Wenye nia (Determined).

4. Kuchukua hatari (Risk taker).

5. Kutatua matatizo (Problem solver).

Mkakati wa Uwekezaji;

Wenye haiba ya Ushindani huwa wanapenda uwekezaji wenye faida kubwa, ambao pia unakuwa na hatari kubwa. Aina ya uwekezaji wanayopendelea zaisi ni hisa zinazokua kwa kasi, ardhi na mali na uwekezaji wa moja kwa moja kwenye makampuni yanayochipukia (startup).

Tahadhari;

Kwa sababu ya kupenda hatari, wenye haiba ya Ushawishi wanaweza kuweka mtaji wao wote kwenye uwekezaji wa aina moja na wanapopata hasara wanaanguka kabisa.

Ili kuepusha hilo, wenye haiba hii wanapaswa kuhakikisha wanatawanya uwekezaji wao kupunguza hatari.

HAIBA YA USHAWISHI (INFLUENCE)

Sifa;

1. Shauku (Enthusiasm).

2. Kuchangamana na wengine (Interactive).

3. Ubunifu (Imaginative).

4. Kusukumwa na hisia (Emotional).

5. Watu wa mitoko (Outgoing).

Mkakati wa Uwekezaji;

Wenye haiba ya Ushawishi wanapenda kufanya uwekezaji unaohusisha watu wengine au kugusa mambo ya kijamii. Huwa ni wazuri kwenye uwekezaji wa vikundi vya pamoja na michezo ya kupeana fedha kwa mzunguko. Pia hupenda kuwekeza kwenye kampuni zinazogusa mambo ya kijamii.

Tahadhari;

Watu wenye haiba ya Ushawishi siyo wazingatiaji sana wa mambo na hupenda kufanya mambo kwa kufuata mkumbo. Kwa sababu wanapenda kuwa kwenye kundi la watu, ni rahisi kusukumwa na kundi kufanya uwekezaji usio sahihi.

Fursa nyingi za kitapeli huwa zinawanasa watu wenye haiba ya ushawishi kwa sababu ya kuongozwa zaidi na hisia na kuamini kinachofanywa na wengi ni sahihi.

Kuepuka hayo, mtu mwenye haina hii anapaswa kuwa anafanya utafiti wa kina kabla ya kuingia kwenye uwekezaji. Na kwa kuwa hili huwa ni gumu kwao, wanapaswa kuwa na washauri sahihi wa kifedha na uwekezaji ili wafanye maamuzi sahihi.

SOMA; Geuza Kibao; Tumia Sababu Zako Za Kutokuwekeza Kupata Msukumo Wa Kuwekeza Zaidi.

HAIBA YA UTULIVU (STEADINESS)

Sifa;

1. Imara (stable/steady).

2. Watulivu (reserved).

3. Kutopenda mabadiliko (resistance to change).

4. Kutabirika (predictable).

5. Uaminifu (loyal).

Mkakati wa Uwekezaji;

Watu wenye haiba ya Utulivu huwa wanapenda vitu vya uhakika na ambavyo ni salama. Hawapendi mabadiliko ya mara kwa mara. Kwenye uwekezaji huwa wanapenda kuwekeza maeneo yenye hatari ndogo na faida ya uhakika, hata kama ni ndogo. Hupendelea zaidi kuwekeza kwenye hatifungani na hisa za makampuni makongwe ambayo yanaaminika. Huwa wanapendelea uwekezaji wa kununua na kushikilia kwa muda mrefu.

Tahadhari;

Wenye haina ya Utulivu hawapendi mabadiliko, hivyo huwa na ukiritimba sana. Hilo linawaweka kwenye hatari ya kupata hasara kwa kushikilia uwekezaji ambao haulipi vizuri. Kwa faida ndogo wanayokuwa wanaipata, mfumuko wa bei unaweza kuiondoa yote. Pia kwa kuogopa hatari, huwa wanakosa kabisa fursa za uwekezaji zinazoweza kuwapa faida kubwa.

Kuepuka hilo, wanapaswa kutawanya uwekezaji wao, badala ya kuweka maeneo yenye hatari ndogo pekee, awekeze na maeneo yenye hatari kubwa yanayoweza kuleta faida kubwa pia.

HAIBA YA UMAKINI (CONSCIENTIOUSNESS)

Sifa;

1. Watiifu (compliant).

2. Waangalifu (Careful).

3. Wachambuzi (analytical).

4. Wenye uwezo (competent).

5. Kutafakari (contemplative)

Mkakati wa Uwekezaji;

Watu wenye haiba ya Umakini huwa wanapenda kufanya utafiti na kuchambua kwa kina kitu kabla ya kuchukua hatua. Hilo huwafanya kutafiti uwekezaji kwa kina kabla ya kuwekeza. Huwa wanapenda kuwekeza kwenye hisa, hatifungani na mifuko ya pamoja inayoonyesha kufanya vizuri.

Tahadhari;

Wenye haina ya Umakini huwa hawachukui hatua kwa haraka mpaka watafiti na kuchambua kwa kina. Hilo huweza kuwapelekea wasiweze kuchukua hatua kabisa, kitu kinachoitwa kupuuza kwa uchambuzi (analysis paralysis). Kwa kuchukua muda mrefu kufanya maamuzi huwa wanakosa fursa nzuri ambazo zinataka maamuzi ya haraka.

Kuondokana na hilo, wenye haiba hii wanapaswa kujipa muda mfupi wa kufanya utafiti na uchambuzi kisha kufanya maamuzi, hata kama wanaona bado hawajatosheka na taarifa. Pale fursa inapokuwa nzuri na utafiti wao wa awali kuona ina faida, wanapaswa kuwekeza mapema badala ya kuchelewa.

Hivyo ndivyo unavyoweza kufanya uwekezaji kwa usahihi kwa kuzingatia haiba yako.

MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA KWA WOTE.

Pamoja na haiba kutofautiana, kuna mambo muhimu ya kuzingatia kwa watu kwenye kufanya uwekezaji na kusimamia utajiri. Mambo hayo ni kama ifuatavyo;

1. Jua Uvumilivu Wako kwa Hatari.

Elewa kiwango chako cha kuhimili hatari na uchague uwekezaji unaolingana na wasifu wako wa hatari. Kama huwezi kuhimili hatari kubwa, usifanye uwekezaji wenye hatari kubwa.

2. Fanya Uwekezaji Mseto.

Bila kujali haiba yako, uwekezaji mseto ni muhimu kwa kudhibiti hatari. Licha ya uwezo wa kuhimili hatari, si busara kuwekeza eneo moja na kuishia kupoteza kila kitu pale hatari inapotokea.

3. Jifunze Endelevu.

Uwekezaji ni kitu kinachotaka kujifunza endelevu ili kupata taarifa za kutosha na kuweza kufanya maamuzi sahihi. Endelea kujifunza na kujinoa kuhusu uwekezaji ili uwe bora.

4. Tafuta Ushauri wa Kitaalamu.

Pamoja na kujifunza endelevu, bado ni muhimu utafute na kutumia ushauri wa wataalamu wa uwekezaji. Hao wanakuwa na ujuzi na uzoefu mkubwa kuliko wewe na siyo rahisi kuathiriwa na haiba zao katika kukushauri. Ni muhimu kupata maoni ya wataalamu kwenye maamuzi yako ya uwekezaji.

Zingatia haya uliyojifunza hapa ili uweze kufanya uwekezaji sahihi kwako bila kuathiriwa na haiba yako.

Karibu kwenye SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2024 ambapo utakwenda kujifunza na kuweka mpango huu kwa vitendo kisha kusimamiwa kwenye kuutekeleza kwa msimamo bila kuacha. Tuma sasa ujumbe wenye maneno SEMINA 2024 kwenda namba 0752 977 175 upate nafasi ya kushiriki semina.

Kitabu kipya cha USIMAMIZI WA FEDHA BINAFSI kina nguzo saba muhimu kwa kila mtu kujijengea ili kuwa imara kifedha. Hiki ni kitabu muhimu kwa kila aliye makini na fedha zake kukisoma. Wasiliana sasa na namba 0752 977 175 kupata nakala yako ya kitabu.

SIKILIZA SOMO HILI KWENYE ONGEA NA KOCHA.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala mzuri wa somo hili ambapo washiriki wamekuwa na maswali na michango mbalimbali. Karibu usikilize hapo chini ili ujifunze na kuchukua hatua sahihi.

MJADALA WA SOMO.

Karibu kwenye mjadala wa somo hili, shiriki kwa kutuma majibu ya maswali haya;

1. Kwa aina nne za watu ulizojifunza kwenye somo hili, unajiona ukiwa kwenye aina ipi zaidi?

2. Aina ya haiba uliyonayo, imekuwa inakuathiri vipi kwenye fedha na uwekezaji? Shirikisha mifano halisi kwako.

3. Baada ya kujifunza kuhusu haiba na uwekezaji, ni maboresho gani unakwenda kufanya kwenye mkakati wako wa uwekezaji?

4. Karibu kwa maswali, maoni, mapendekezo na shuhuda kuhusu somo hili na programu nzima ya NGUVU YA BUKU na UHURU WA KIFEDHA.

Tuma majibu ya maswali hayo kama uthibitisho wa kusoma, kuelewa na kutekeleza somo hili la uwekezaji.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.