3545; Yasiyo Ya Kawaida.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Ili upate mafanikio makubwa unayoyataka kwenye maisha yako, ni lazima ufanye vitu ambavyo hujawahi kufanya.
Na siyo tu ambavyo wewe hujawahi kufanya, bali pia vile ambavyo wengi wanaokuzunguka hawajawahi kufanya.
Na kwa uhakika kufanya hivyo kutapelekea uonekane mtu wa ajabu, kwa sababu unayofanya siyo ya kawaida.
Kama unataka kujenga biashara kubwa, ambayo wote wanaokuzunguka hawajawahi kujenga, hupaswi kuwa kama wao walivyo.
Hupaswi kufanya mambo yako kama wao wanavyofanya mambo yao.
Hupaswi kusikiliza hata ushauri wao.
Kwa sababu kitu pekee wanachokuwa wanataka kufanya ni kuhakikisha huwi tofauti na wao.
Watakuambia mengi sana kuhusu safari ya mafanikio unayokuwa umeichagua.
Lakini yote hayana mchango kwako, kwa sababu hayajawa na mchango kwao wenyewe.
Kujenga mafanikio makubwa sana kuliko ilivyozoeleka kunakutaka ujitoe sana.
Kunakutaka uwe na maisha ambayo yataonekana siyo ya afya.
Watu watakuambia unapaswa kuwa na mlinganyo au usawa wa maisha na kazi.
Lakini uhalisia ni kazi itahitaji upendeleo zaidi kuliko maisha, kama unataka kufanya makubwa.
Mafanikio makubwa yanakutaka ujitoe mazima kwenye kile ulichochagua kupambania.
Hupaswi kugawa nguvu, muda na umakini wako kwenye kitu kingine chochote.
Nguvu kubwa sana inahitajika kukutoa pale unapokuwa na kukupeleka kwenye mafanikio makubwa zaidi.
Na wakati huo unaweka nguvu ya kwenda juu, kuna nguvu nyingine kubwa inayokuwa inakuvuta chini.
Juhudi zozote unazodhani wewe zitakufikisha kwenye mafanikio makubwa ni ndogo sana ukilinganisha na uhalisia.
Hata kama tayari unaona unaweka juhudi kiasi gani, kama bado hujafika kule unakotaka, juhudi bado hazijatosha.
Badala ya kubishana na watu au kutaka kuonekana kwa namna fulani na watu, ni vyema ukapeleka nguvu hizo kwenye kufanya yasiyo ya kawaida ili upate mafanikio.
Mafanikio makubwa siyo kwa ajili ya kila mtu.
Bali ni kwa wachache waliojitoa kafara kupata kile hasa wanachotaka.
Ambao hawaruhusu chochote kile kiwakwamishe.
Rafiki, je wewe ni mtu wa aina hiyo?
Umejitoa kiasi gani katika kufanya yasiyo ya kawaida ili upate mafanikio makubwa?
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe