3547; Jinsi ya kutokwamishwa na wengine.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye safari ya mafanikio, unalazimika kufanya mambo ambayo hujawahi kufanya.
Ambayo hata wanaokuzunguka hawajawahi kufanya.
Hilo halitakupa utulivu hata kidogo, kwa sababu hayo ambayo hujawahi kufanya yanakuwa magumu kwako.
Na ugumu zaidi unaletwa na wengine, ambao watakufanya uone unakosea kwa kujaribu kufanya tofauti na ilivyozoeleka.
Kwa maoni ambayo wengine wanakuwa nayo kwako, pamoja na matokeo unayokuwa unapata, ambayo ni tofauti kabisa na matarajio, unaweza kuona wako sahihi.
Unaweza kushawishika usihangaike kufanya hayo ya tofauti, badala yake urudi kwenye mazoea.
Huo huwa ndiyo mwisho wa ndoto kubwa wanazokuwa nazo watu wengi.
Wanakubali kukwamishwa na wengine na matokeo wanayopata.
Kwa sababu mambo yanakuwa mapya na magumu kwao, wanaona watu hao wengine wako sahihi kuliko wao.
Ili kuepuka kukwamishwa na yeyote au chochote pale unapoamua kupata mafanikio makubwa, kuna misingi mitatu unayopaswa kuzingatia.
Msingi wa kwanza ni mara zote kuchukua hatua zinazoifanya dunia kuwa sehemu bora zaidi ya kuishi.
Kila unachofanya, hakikisha kinakuwa na mchango mzuri kwa dunia. Kinaifanya dunia kuwa sehemu bora zaidi ya kuishi kwa wote.
Hapa unafanya lile lililo sahihi kwa wengi, hata kama baadhi hawaoni hilo mapema.
Msingi wa pili ni kutokufanya chochote kinachowakwamisha wengine kufikia malengo yao.
Kwa kila unachofanya, hakikisha huwi kikwazo kwa wengine kupata au kufika kule wanakotaka kufika.
Hapa unapaswa kuwa na mtazamo wa utele, kwamba dunia inaweza kuwapa watu wote yote wanayotaka hivyo hakuna haja ya kuzibiana riziki.
Msingi wa tatu ni kufanya kila kinachohitajika kufanyika ili kupata unachotaka.
Hapa unapaswa kujitoa kwa kila namna ili kufikia malengo uliyonayo. Hufanyi kile kilicho ndani ya uwezo wako au unachoweza kufanya, bali unafanya kila kinachopaswa kufanyika.
Kwa kuzingatia misingi hiyo mitatu, utaweza kujisukuma kupata chochote unachotaka bila kukubali kukwamishwa na mtu yeyote yule.
Wala hutahofia kwamba kufanya kwako kwa msukumo mkubwa kunakuwa kikwazo kwa watu wengine.
Unapofanya kile kilicho sahihi kwako kwenye kupata unachotaka na chenye manufaa kwa wengine na dunia kwa ujumla, hupaswi kukubali chochote kikuzuia kufika kule unakotaka.
Mafanikio ya kweli kwenye maisha ni mtu kupata kile unachotaka, bila ya kujali umepitia nini.
Unaweza kuwa na sababu nzuri sana kwa nini hujaweza kupata unachotaka, lakini sababu hizo hazitafanya uwe umefanikiwa.
Kama hujapata unachotaka, hujafanikiwa, hata ujipe sababu nzuri kiasi gani.
Fanya kila kinachohitajika kufanyika ili uweze kupata unachotaka.
Hilo siyo tu litakupa mafanikio makubwa, bali pia litakuonyesha uwezo mkubwa ulio ndani yako ambao hukuwahi kujua kama unao au kuweza kuutumia.
Rafiki, ni msukumo gani mkubwa unaotoka nao hapa kuhakikisha unapata kila unachotaka kwenye maisha yako bila kukwamishwa na wengine?
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe