3548; Kudhalilishwa na maisha.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Watu wamekuwa wanahangaika kutafuta hamasa za nje za kupambana kufanikiwa.
Hiyo ni kwa sababu hamasa ni sehemu muhimu sana ya mafanikio yoyote yale.
Lakini changamoto kubwa ya hamasa kutoka nje ni huwa hazidumu.
Mtu anaweza kupata hamasa kwa kusoma au kusikiliza wengine.
Akatoka akiwa na msukumo wa kwenda kufanya makubwa.
Lakini baada ya muda mfupi hamasa hiyo huisha na kujikuta wakirudi kwenye mazoea yao.
Licha ya hamasa hizo za nje kutokuwa na manufaa, bado watu wengi sana wanakimbizana nazo kila siku.
Watu wanahangaika kupata hamasa hizo za nje siyo kwa sababu zina manufaa yoyote kwao, bali kwa sababu zinawafanya wajisikie vizuri.
Tunachojua kwa uhakika kabisa ni hayupo mtu aliyeweza kufanya makubwa kwa kutegemea hizo hamasa za nje.
Wote ambao wameweza kufanya makubwa sana walikuwa na hamasa ya ndani.
Na hamasa ya ndani yenye nguvu isiyoisha huwa inatokana na kudhalilishwa na maisha.
Ni pale mtu anapopitia hali ambayo inamdhalilisha sana ndiyo anakata shauri kwamba kamwe hatakuja kukubali kudhalilika tena hivyo.
Kudhalilika huko kunampa hasira inayomsukuma kufanya makubwa kwenye maisha yake.
Pale hamasa inapopungua, mtu akikumbuka tu udhalilishaji aliopitia, hamasa inajichochea upya.
Kudhalilishwa na maisha ni hamasa ambayo huwa haipoi.
Ukiwa nayo na ukaitumia vyema, utapata msukumo wa kufanya makubwa sana.
Rafiki, ni kwa namna gani maisha yamewahi kukudhalilisha mpaka ukaapa kwamba hutakuja kuruhusu hilo kutokea tena?
Tumia hilo kama hamasa itakayokusukuma bila kuchoka.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe