3554; Okoa Pesa Zako.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Pesa zako zinawindwa sana.

Jinsi wewe unavyopambana kupata pesa, ndivyo pia na wengine wanavyopambana kukutenganisha wewe na pesa zako.

Katika mapambano hayo ambayo wengine wanayaendesha kupata pesa zako, wana mbinu kali sana za ushawishi.

Usipojua na kuweza kukwepa mbinu hizo, kamwe hutakuja kukaa na pesa unazopata.
Kila utakapopata pesa utaona kuna matumizi muhimu unayopaswa kuyakamilisha.

Kwa kuwa mbinu za ushawishi ni nyingi, siyo rahisi kuwa na njia ya kuvuka mbinu moja moja.

Lakini uzuri kuna njia moja ya kuvuka mbinu zote za ushawishi wa matumizi ya pesa zako.
Kwa kutumia njia hiyo moja, unakuwa na uwezo wa kuzuia matumizi yote nyemelezi yanayoletwa na wanaowinda pesa zako.

Njia hiyo ina hatua tatu muhimu;
1. Nunua kitu ambacho una matumizi nacho.
2. Kitumie kitu hicho mpaka kife au kiwe hakiwezi tena kutekeleza matumizi.
3. Ndipo ununue kitu kingine.

Ukifuata mtiririko huo rahisi sana, utaokoa fedha nyingi ambazo umekuwa unapoteza kwa ushawishi wa wauzaji mbalimbali.

Tuangalie mfano rahisi wa simu.
Makampuni ya simu huwa yanakuja na toleo jipya la simu kila mwaka.
Kila toleo jipya huwa linapambwa sana kwamba ni muhimu mtu alipate.
Na hiyo imekuwa inapelekea watu kuingia gharama kubwa mara kwa mara kwenye manunuzi ya simu.

Kwa kutumia mtiririko tuliojifunza hapa, unapaswa;
1. Kununua simu ambayo inakamilisha matumizi uliyonayo.
2. Tumia simu hiyo mpaka itakapokufa, au kuwa haitimizi tena majukumu yako.
3. Ndipo ununue simu nyingine.

Ukifuata huo mtiririko, kamwe hutanunua siku kila mwaka, itakuchukua muda mrefu kununua siku na utaokoa fedha nyingi.

Huo ni mfano mmoja wa simu, lakini ndivyo inavyopaswa kuwa kwenye kila matumizi unayofanya kwa fedha zako.

Rafiki, ni mara ngapi umenasa kwenye matumizi ambayo baadaye unakuja kujutia kwa sababu hayakuwa muhimu kama ulivyoshawishiwa?
Kuanzia sasa usikubali tena kuhadaiwa, tumia mtiririko uliojifunza hapa kuepuka kutenganishwa na pesa zako kizembe.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe