3555; Ongoza njia kuwapata walio sahihi.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye safari ya mafanikio, tunawahitaji sana watu walio sahihi wa kushirikiana nao.
Lakini kuwapata watu sahihi imekuwa siyo zoezi rahisi.
Unaweza kukazana sana kuwaambia watu kile unachotaka na kule unakotaka kufika, lakini bado itakuwa vigumu kuwapata walio sahihi.
Kuna watu watajaribu kukushawishi kwamba wao ni sahihi kwa maneno, lakini inapofika kwenye kufanya kwa vitendo, unagundua siyo sahihi.
Unaweza usijue tatizo ni nini, lakini kwa sehemu kubwa tatizo ni la watu wenyewe kukosa kujiamini wao wenyewe.
Kujaribu kuwashawishi watu ambao hawajiamini wao wenyewe watake kufanya makubwa zaidi ni kujidanganya tu.
Kama unataka kupata watu sahihi wa kushirikiana nao ili kupata mafanikio makubwa unayoyataka, acha kuhangaika na kuwashawishi kwa maneno.
Acha kuwashawishi watu ambao hawajiamini hata wao wenyewe wawe na msukumo wa kufanya makubwa.
Ni kitu ambacho hata ndani yao tu hawajioni wakiwa hivyo.
Unachopaswa kufanya ni kuongoza njia kwa kufanya yale yanayohitajika kufanyika.
Wewe unaanza kuwa mfano wa kile kinachopaswa kufanyika na unafanya kwa viwango vya juu kabisa unavyovitaka.
Ni kupitia kufanya ndiyo utaweza kuwavutia watu sahihi. Wale wanaoweza kufanya vile unavyofanya wewe watavutiwa kuungana na wewe.
Watu unaowapata kwa njia hii wanakuwa bora, kwa sababu wanakuwa ni wafanyaji kweli na siyo wasemaji tu.
Kama unahangaika na hupati watu sahihi, jua kabisa kwamba wewe hujawa sahihi.
Unaweza kusema sana, lakini kama hujafanya, utakaowapata hawatakuwa sahihi.
Kuwa vile unavyotaka watu wawe na utaweza kuwavutia watu wa aina hiyo.
Tofauti na wengi wanavyojua na kuamini, watu huwa hawatengenezwi, bali huwa wanavutiwa.
Watu tayari wako vile walivyo, unachoweza kufanya wewe ni kuchuja ili kupata walio sahihi kwako.
Na mchujo sahihi ni kwa wewe kuongoza njia kwa kufanya, kwa viwango vya juu ambavyo ndiyo unataka wengine pia wawe wanafanya.
Rafiki, ni watu wa aina gani umekuwa unawatafuta sana lakini huwapati?
Je umeshafanya vile unavyotaka unaowatafuta wawe wanafanya?
Anza kwa kuongoza njia kwenye kila eneo unalotaka kupata watu sahihi na utawapata.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe