3558; Kukaa kwa kutulia.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Kipindi cha nyuma, mafanikio makubwa yalikuwa yanahitaji mtu kuwa na akili kubwa.

Lakini kwenye zama hizi, mafanikio hayahitaji akili kubwa sana.
Kwa sasa kuna mifumo inayoweza kuchakata mambo mengi kwa haraka kuliko mtu yeyote.

Kinachohitajika ni mtu kuweza kutoa maelekezo sahihi kwenye mifumo iliyopo kisha kupokea majibu sahihi kutoka kwenye mifumo hiyo.

Kwenye zama hizi, mafanikio makubwa yanahitaji mtu kuwa na utulivu mkubwa sana. Yanataka mtu kuweza kukaa kwa utulivu na kuweka umakini wake kwenye vitu vichache muhimu badala ya kuhangaika na mengi ambayo siyo muhimu.

Changamoto kubwa ya zama hizi ni usumbufu na kelele zenye ushawishi mkubwa kwa watu.
Kila wakati kuna fursa nyingi mpya zinazojitokeza. Fursa hizo zinashawishi sana mtu kuzichangamkia ili kunufaika.

Lakini pale unapofanya hivyo, unaishia tu kupoteza rasilimali zako na kuja kugundua mambo siyo rahisi kama yanavyoonekana na kuelezewa.

Chochote ambacho mtu anafanya kinaweza kumfikisha kwenye mafanikio makubwa.
Lakini hilo litawezekana kama mtu utaweza kukaa kwa utulivu kwenye ufanyaji wa kitu hicho na kutokuvurugwa na mengine mazuri yanayojitokeza.

Hiyo inakwenda mpaka kwenye umakini wakati wa kufanya jambo.
Kama huwezi kuweka umakini wako wote kwenye lile unalokuwa unafanya, huwezi kulifanya kwa ubora wa juu unaohitajika ili ufanikiwe.

Ni lazima uweze kukaa kwa utulivu na kukamilisha majukumu yako bila kuruhusu usumbufu wa aina yoyote ile kukuathiri.

Rafiki, je unaweza kuziba masikio na kufumba macho kwenye fursa mpya zinazojitokeza kila mara ili uweke umakini wako wote kwenye kile ulichochagua kikutoe?
Hapo ndipo penye mtihani mkali ambao ukiweza kuuvuka, mafanikio ni yako kwa uhakika.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe