3569; Ushauri utakaokusaidia.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye safari ya mafanikio, watu wamekuwa wanaomba ushauri na kujifunza mambo mbalimbali.
Lakini ushauri na hayo wanayojifunza yamekuwa hayawasaidii, siyo kwa sababu hayawezi kuwasaidia, bali kwa sababu watu hawayafanyii kazi.
Na watu wamekuwa hawafanyii kazi ushauri na mafunzo wanayopata kwa sababu ya ujuaji.
Unakuta mtu anashauriwa au kujifunza kitu, halafu anajiambia kwake hakitafanya kazi, kabla hata hajakifanyia kazi.
Matokeo yake ni mtu kujikuta akiwa anakataa kila kitu na kutokufanya chochote cha tofauti.
Anakuwa anashauriwa na kujifunza mengi, lakini anayokuwa anafanya ni yale yale ambayo amekuwa anafanya mara zote.
Sote tunajua kwamba huwezi kupata matokeo ya tofauti kama utaendelea kufanya mambo yale yale kwa namna ile ile.
Ushauri na mafunzo yatakayokusaidia ni yale utakayoyafanyia kazi moja kwa moja.
Unaposhauriwa au kujifunza kitu chochote, usianze kukihukumu kama kitafanya au hakitafanya kazi kwako.
Badala yake kifanyie kazi kama ulivyoshauriwa au kufundishwa.
Fanya kila ulichojifunza, kwa jinsi ulivyojifunza.
Kisha tathmini matokeo unayokuwa umeyapata, angalia yale yanayofanya kazi kwako na endelea nayo.
Yale yasiyofanya kazi ndiyo unaachana nayo.
Utajua nini kinafanya kazi kwako na nini hakifanyi kazi kwa kufanyia kazi.
Hukumu yako inapaswa kuwa ni baada ya kufanyia kazi vitu na siyo kabla.
Kuna kitu unachoweza kujifunza kutoka kwa kila mtu.
Lakini vitakavyokusaidia ni vile utakavyofanyia kazi tu.
Kila kitu kinafanya kazi, kama kitafanyiwa kazi.
Utasumbua sana watu,
Utawasema vibaya wanaokushauri na kukufundisha,
Kwa uzembe wako mwenyewe wa kutokufanyia kazi yale unayoambiwa.
Rafiki, hebu pata picha kama ungefanyia kazi kila ushauri na mambo ambayo umeshajifunza, ungekuwa mbali kiasi gani?
Ni wakati sasa wa kuweka kiburi pembeni na kuweka kwenye matendo yale yote unayojifunza ili yaweze kuwa na manufaa kwako.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe