3570; Fanya kinyume.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Kwenye safari ya mafanikio, wengi wamekuwa wanalalamika kukosa watu sahihi wa kujifunza kutokabkwao ili waweze kufanikiwa.

Na tunaijua nguvu ya wale wanaotuzunguka, jinsi ambavyo tunaishia kuwa kama wao na kufanya yale wanayokuwa wanafanya.

Pamoja na hayo yote, bado kila mtu anaweza kupata mafanikio makubwa hata kama amezungukwa na ambao hawajafanikiwa.
Ila ndiyo inahitaji nguvu ya ziada ili mtu kuweza kupata mafanikio makubwa kama amezungukwa na ambao hawajafanikiwa.

Kinachohitajika ili mtu kuweza kupata mafanikio makubwa ni kufanya kinyume na wanavyofanya wale wanaomzunguka.
Kwa sababu mtu anakuwa amezungukwa na wengi ambao hawajafanikiwa, anachopaswa kufanya ni kuangalia yale ambayo watu hao wanayafanya kisha yeye kufanya kinyume chake.

Utaweza kupata ukuaji mkubwa kimafanikio kwa kuchukua yale ambayo watu wa kawaida wanayafanya kisha kufanya kinyume chake.

Kama pale walipo wengi wanaokuzunguka siyo unapotaka kuwa, unapaswa kufanya tofauti na wanavyofanya wao.

Hilo siyo tu linahitaji mtu kuwa na utayari wa kuwa tofauti, bali pia linataka mtu kuwa na ujasiri na kutokujali sana wengine wanamchukuliaje.

Kwa sababu mtu atakapoanza kufanya kinyume na wengine, hawatamwacha salama.
Watamwona ni mtu mkaidi, anayevunja sheria na kukosa usawa kwa wengine.
Yaani watu wamekaa kwenye mazoea mpaka wanayachukulia kama ndiyo sheria na haki.
Ukienda kinyume na mazoea nayo, unaonekana ni msaliti, usiyejali na usiye na usawa.

Hayupo mtu yeyote, kwenye historia ya dunia, amewahi kupata mafanikio, kwenye jambo lolote lile, kwa kufuata mazoea na kumridhisha kila mtu.

Fuatilia kila aliyefanikiwa na utaona jinsi ambavyo amekutana na upinzani mkali kutoka kwa wale wanaomzunguka.
Yote hayo yanakuwa yanasababishwa na uthubutu wa watu hao kwenda kinyume na mazoea yaliyopo, ambayo watu wameshachukulia ndiyo sheria na utaratibu.

Rafiki, ni mara ngapi umekuwa unajaribu kufanya mambo ya tofauti, ila ukapingwa sana na wanaokuzunguka mpaka ukaamua kuacha?
Kama unataka mafanikio makubwa sana, zaidi ya wote wanaokuzunguka, moja, lazima ufanye kinyume na wanavyofanya wao.
Na mbili, usijali watu wanakuchukuliaje kwa hayo ya tofauti unayofanya. Utapingwa sana, lakini jua hiyo ni sehemu ya safari, hivyo endelea.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe