3572; Jinsi ya kuwa mtu hatari.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Watu ambao huwa wanapata kile wanachotaka mara zote, huwa wanaonekana ni watu hatari zaidi.

Hiyo ni kwa sababu sehemu kubwa ya watu huwa hawapati wanachotaka.

Yaani yale yote ambayo unaona watu wengi wanayo sasa, siyo hasa waliyokuwa wanataka.
Walijikuta wanakubaliana na hayo waliyopata baada ya kukosa yale hasa waliyotaka.

Kazi ambazo wengi wanazofanya, siyo kazi ambazo wanazipenda zaidi. Bali ni kazi walizoweza kupata na zinazowawezesha kuendesha maisha.

Biashara ambazo wengi wanafanya, siyo ndiyo wanazopenda zaidi, bali ndiyo zinazoweza kuwalipa.
Kiasi ambacho watu wanapata kutoka kwenye biashara wanazofanya siyo ndiyo kiasi ambacho wangependa kupata, lakini wameridhika nacho kwa sababu hawajaweza kupata wanachotaka.

Kama unataka kuwa mtu hatari, ambaye unapata kila unachotaka, kwa namna unavyotaka, kuna kitu kimoja tu unapaswa kufanya.
Kitu hicho ni utayari wa kuanza upya mara zote.
Bila ya kujali umekutana na nini, unapokosa ulichotaka, unaanza upya mchakato wa kuhakikisha unakipata.

Ukishaamua unataka kitu, umemaliza, kinachofuata ni wewe kufanya mpaka ukipate.
Hata ukutane na nini, wewe unaendelea na safari yako.
Ukikutana na kikwazo chochote unakivuka na kuendelea.
Ukipotea njia, unarudi kwenye njia kuu na kuendelea.
Ukishindwa, unaanza tena upya.

Hebu fikiria utakuwa mtu wa aina gani kama utaendelea kupambania kile unachotaka bila kuzuiwa na chochote?

Dunia yenyewe itasalimu amri na kukupa kile unachotaka, kwa namna unavyotaka.
Unakuwa mtu hatari, uliyeshindikana, lakini unayepata kile unachotaka.

Rafiki, kuwa mkweli kwako kwenye kujijibu swali hili; hapo ulipo sasa, ndipo hasa ulipotaka kuwa? Kama jibu ni hapana, amua sasa kuwa mtu hatari sana. Rudi kwenye kupambania kile hasa ulichotaka bila kukubali kukwamishwa na kitu chochote kile.

Unapoendelea kupambania unachotaka, bila kukubali kukwamishwa na chochote, unakuwa mtu hatari na kuweza kupata kila unachotaka.
Hakuna kinachokuzuia wewe kuwa hatari, amua sasa ili uweze kuwa na maisha ya ndoto yako.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe