3573; Nani anauza?
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Ukuaji na mafanikio ya biashara inategemea na nani anayeuza.
Unapoanza biashara, wewe ndiye unayeuza.
Hata kama una watu wanaokusaidia majukumu ya biashara, bado wewe ndiye unayekuwa muuzaji mkuu.
Hilo ni zuri wakati wa kuanza, kwa sababu wewe ndiye unayekuwa unaiamini bidhaa/huduma yako kuliko mtu mwingine yeyote.
Lakini huwezi kukuza biashara na kupata mafanikio makubwa kama utabaki kwenye ngazi hiyo.
Kwani hata uwe muuzaji bora kiasi gani, kuuza mwenyewe kuna ukomo. Kuna wateja wengi ambao hutaweza kuwafikia.
Hilo linatupeleka kwenye ngazi ya pili ya mauzo ambayo ni pale timu yako inapouza.
Kwenye ngazi hii unakuwa na ukuaji na kuwa na wauzaji wengi badala ya wewe peke yako.
Kuwa na timu ya mauzo kunaondoa ukomo wa wewe kuwa muuzaji pekee.
Ili timu iweze kuuza vizuri, lazima kuwe na mfumo mzuri wa mauzo na biashara kwa ujumla na watu kwenye timu hiyo kuwa bora.
Biashara haiwezi kufanya mauzo makubwa kwa kuchukua tu mfanyakazi yeyote na kila mfanyakazi kujiamulia auzeje.
Lazima timu ya biashara iwe na watu bora sana waliofanyiwa mchujo. Kisha kupewa miongozo sahihi na ya uhakika inayoleta mauzo makubwa.
Kuwa na timu ya mauzo siyo mwisho, kwani na yenyewe huwa inafikia ukomo. Pamoja na kuwa na wauzaji wengi, bado kuna wateja hawataiamini biashara yako kwa sababu hawajawahi kununua.
Hilo linapelekea kuwepo na ngazi ya juu kabisa ya mauzo, ambayo ni pale wateja wako wanapouza bidhaa/huduma yako.
Kwenye ngazi hii, wateja wanatoa shuhuda nzuri na kuwaambia watu wengine waje kununua.
Ukiisifia biashara yako wewe mwenyewe, watu watasema unajisifia na kujipendelea.
Lakini wengine wakiisifia biashara yako, inachukuliwa ni sifa za kweli.
Pia watu wanawaamini wale wanaowajua kuliko wasiowajua.
Hivyo wateja wanaposifia biashara yako, watu wao wa karibu wanaiamini hata kama hawakujui wewe.
Ngazi ya wateja kuuza biashara yako ni kubwa, lakini siyo ya juu kabisa.
Kwani ipo ngazi ya juu zaidi, ambayo ni biashara kujiuza yenyewe.
Biashara inakuwa inajiuza yenyewe pale jina la biashara linapotumika kama kitendo na/au kivumishi.
Kwa mfano mtu badala ya kusema anatafuta kitu mtandaoni, anasema ana google. Google ni jina la bidhaa/huduma, lakini linachukuliwa kama kitendo.
Kadhalika majina kama sheli, pampas, kiwi na colgate ni majina ya bidhaa ambayo yamekuwa yanatumika kama kitendo.
Biashara inajiuza yenyewe pale inapokuwa imejijengea jina linaloaminika na kukubalika (brand).
Na hayo ni matokeo ya biashara kuendeshwa kwa misingi sahihi na inayosimamiwa mara zote.
Kila biashara inayo fursa ya kufika ngazi hiyo ya juu, japo inatumia muda mrefu.
Rafiki, kwenye biashara yako, nani ndiye muuzaji kwa sasa? Wewe, timu, wateja au biashara yenyewe?
Jua ngazi uliyopo kisha chukua hatua sahihi kwenda ngazi ya juu zaidi ya uliyopo.
Unapofika ngazi ya juu kabisa unakuwa hujamaliza, kwani unapaswa kutunza na kubaki kwenye nafasi hiyo.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe