3574; Utazidi kupitwa.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye safari ya mafanikio, utakutana na watu wengi sana ambao nao wanapambana kufanikiwa.
Na kuna wengi ambao watakuwa mbele yako kwenye chochote unachofanya.
Watu hao wanakuwa wamekuzidi kwenye hatua walizopiga.
Kwa kifupi, wanakuwa wanapata ushindi zaidi yako.
Jinsi utakavyowachukulia wale waliokuzidi ndiyo itakavyoamua kama utafanikiwa au utashindwa.
Watu huwa wanawachukulia waliowazidi kwa namna tatu.
Moja ni kuona watu hao hawastahili.
Hapa watu hutafuta kitu ambacho kimewapa watu hao upendeleo wa kufanikiwa kuliko wao.
Watasema ni kwa sababu wametokea familia yenye uwezo, au walisaidiwa, au wameiba na mengine mengi.
Wanaowachukulia waliofanikiwa kwa namna hii hujaribu kuonyesha watu hao hawajashinda kwa uwezo wao.
Na hilo haliwasaidii chochote wao.
Mbili ni kutaka kuwaangusha wale waliofanikiwa.
Hapa wanaopitwa kimafanikio wanapatwa hasira, chuki na wivu na hisia hizo hasi kuwasukuma wawaangushe waliowazidi.
Hisia hasi huwa zina nguvu kali na humteka mtu afanye uharibifu.
Kumharibia aliyefanikiwa hakujawahi kumpa ushindi yule ambaye hajafanikiwa.
Tatu ni kutaka kumzidi aliyefanikiwa.
Hapa aliyepitwa anajiambia kama yeye ameweza, hata mimi ninaweza.
Anajiuliza ni vitu gani vilivyompa ushindi yule aliyeweza.
Wanajijengea vitu hivyo ili nao waweze.
Wanajifunza kwa waliofanikiwa, ili nao waweze kufanikiwa.
Na hilo linawapa mafanikio makubwa sana.
Rafiki, mpaka sasa naamini umeshaona ni njia ipi unapaswa kuifuata wewe ili ufanikiwe.
Njia yenyewe ni kutaka kufanikiwa zaidi ya waliokutangulia.
Kama utachukua njia ya kuona waliokuzidi hawastahili au unapaswa kuwaangusha, jua utazidi kupitwa.
Unapaswa kupeleka rasilimali zako zote kupata mafanikio makubwa zaidi ya wengine wote waliokutangulia.
Mengine tofauti na hapo hayakuhusu kabisa.
Rafiki, ni watu gani waliofanikiwa kukuzidi ambao unajifunza kwao ili uweze kufanikiwa zaidi yao?
Kaa kwenye mtazamo huo wa kufanya zaidi ya wengine ili upate ushindi mkubwa kwenye maisha yako.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe