3575; Hivi unajijua kweli?
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Watu huwa wanahangaika sana na siri za mafanikio, wakati hatua ya kwanza na ya msingi kuelekea kwenye mafanikio bado hawajaipiga.
Ni sawa na mtu anayehangaika na ngazi ya kumi, wakati hata ngazi ya kwanza bado hajaipiga.
Au mwanafunzi anayetaka kufanya mtihani wa darasa la saba, wakati hajaanza hata darasa la kwanza.
Miaka mingi sana iliyopita, kwenye hekalu la Apollo, sehemu iliyokuwa na hekima zaidi, paliandikwa; KNOW THYSELF. Ikiwa na maana; JIJUE WEWE MWENYEWE KWANZA.
Naye Socrates, baba wa falsafa, mtu aliyekuwa na hekima zaidi alikuwa akiwasisitiza watu; Kujijua mwenywe ndiyo chanzo cha hekima.
Unaweza kusema; “Kocha bana, mbona mimi najijua tayari?”
Sitakukatalia juu juu, bali nitakuomba unijibu maswali haya;
1. Wewe ni nani?
2. Uko hapa duniani kufanya nini?
3. Ukiondoka, dunia itakosa nini?
Kama majibu yako ni…
1. Mimi ni … (Jina lako)
2. Niko hapa duniani kuishi.
3. Nikiondoka dunia itakosa uwepo wangu.
… bado hujajijua.
Hatuishii hapo, twende kwenye kazi au biashara unayofanya.
Kutokujijua wewe mwenyewe inakuzuia hata kufanikiwa kwenye kazi na biashara.
Na kama unadhani unajijua, hebu jijaribu hapa;
1. Kwa nini unafanya kazi/biashara unayofanya?
2. Nini kinatofautisha kazi/biashara yako na za wengine?
3. Kwa nini wengine waache kote na kuja kwako?
Kama huwezi kuyajibu hayo kwa uwazi kabisa, siyo tu hujijui, bali pia hujui unachofanya.
Na hapo mafanikio yatakuwa magumu sana kwako.
Rafiki, je unajijua wewe mwenyewe kwa undani kabla hujaendelea kupambana na mafanikio?
Kama bado hujajijua, basi hiyo ndiyo kazi kubwa iliyo mbele yako kwa sasa.
Ikamilishe kabla hujaendelea na mengine.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe