3576; Tofautisha marafiki na wateja.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye safari ya mafanikio, mauzo ni kitu muhimu sana.
Unahitaji kuwashawishi watu wengine wakubaliane na wewe ili kukupa kile unachotaka.
Mahali ambapo wengi wanakwama ni kushindwa kutimiza pande hizo mbili; KUKUBALIKA na KUPATA UNACHOTAKA.
Watu wengi huhangaika na kukubalika na wengine, na hilo wanalipata kwa uhakika.
Lakini wanashindwa kupata wanachotaka na hilo kuwapelekea kushindwa.
Rafiki, inapokuja kwenye safari ya mafanikio, kuna marafiki na kuna wateja.
Marafiki ni wale wanaokukubali sana, wanakuelewa na wapo tayari kukupambania.
Lakini wanakuwa hawana uwezo wa kukupa kile unachotaka.
Wanaikubali sana biashara yako, lakini hawawezi kumudu kulipia unachouza.
Hao ni marafiki, watu wazuri kabisa na hawana tatizo lolote.
Wateja ni wale wanaokukubali na wanaweza kukupa unachotaka.
Wateja wanaweza kumudu kununua kile unachouza.
Hao ndiyo watakaokuwezesha wewe kupata unachotaka ili kufikia mafanikio makubwa.
Unaweza kuwa na marafiki wengi sana, wanaokukubali na kukutakia mema ufanikiwe.
Lakini wakawa hawana uwezo wa kununua unachouza.
Tunachopaswa kujifunza hapa siyo kuwapuuza marafiki, bali kujenga biashara zetu kwenye misingi sahihi.
Jenga biashara yako tangu awali ukiwa unajua mteja halisi ni nani na ataiwezeshaje biashara pamoja na wewe kufanikiwa.
Usijenga biashara kwa kuangalia marafiki, utaishia njiani.
Rafiki, je unaowalenga sasa wana uwezo wa kumudu kulipia unachouza?
Kama jibu ni ndiyo, hao ni wateja, weka kazi kuwafikia wengi wa aina hiyo.
Kama jibu ni hapana, hao ni marafiki, badili mwelekeo wa biashara yako kabla haijafa.
Jenga biashara kwa kulenga wateja na siyo marafiki, itakuwezesha kuwa na biashara yenye mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe