3579; Muda na Pesa.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Muda na pesa ni vitu viwili ambavyo vimekuwa vinachanganywa sana na wengi.
Wengi wanachanganya hivi, mahali pa kuweka muda wao wanaweka pesa.
Na mahali pa kuweka pesa wao wanaweka muda.
Kushindwa kuweka muda na pesa kwenye maeneo sahihi imekuwa kikwazo kwa wengi kupiga hatua kubwa kwenye maisha yao.
Unakuta mtu anatumia muda ili kuokoa pesa, wakati muda ukishapita haurudi tena.
Leo nataka tushirikishane namna sahihi ya kupangilia muda na pesa ili kufanya makubwa.
Unapaswa kuweka pesa kwenye vitu unavyovielewa na kuweka muda kwenye vitu ambavyo huvielewi.
Hiyo ni sentensi iliyobeba maana kubwa sana, ambayo ukiielewa utafanya makubwa sana.
Tuanze na sehemu ya kwanza; WEKA PESA KWENYE VITU UNAVYOELEWA.
Kazi ya pesa ni kukuza vitu, kukupa matokeo makubwa kwa juhudi kidogo.
Pesa itakuwa na matokeo mazuri kama utaiweka mahali ambapo unapaelewa vizuri.
Ndiyo maana hata kwenye mtaji wa biashara, taasisi za fedha hazikupi mkopo wa biashara kama unaenda kuanza.
Watakuambia ufanye kwa miezi sita mpaka mwaka kwanza.
Kwa sababu wanajua, unapoanza kitu, hujui. Kuweka pesa kwenye kitu ambacho hujui ni njia ya uhakika ya kuipoteza.
Tukienda sehemu ya pili; WEKA MUDA KWENYE VITU AMBAVYO BADO HUJAELEWA.
Unahitaji muda kuelewa vitu ili uweze kunufaika navyo.
Kwa bahati mbaya sana hiyo hatua huwa haina njia ya mkato.
Ni lazima uweke muda kujifunza na kuelewa kwa kina.
Hapo ndipo unaweza kunufaika.
Rafiki, umeonajua sasa kwa nini umekuwa unakwama, ni kuchanganya hayo mawili.
Unaweka pesa kwenye vitu usivyoelewa na kuishia kuzipoteza, huku ulipoteza muda kwenye vitu ambavyo umeshavielewa.
Usiendelee kujikwamisha tena.
Unapokuwa unaanza kitu kipya, jipe muda wa kujifunza na kukielewa kwa kina.
Ukishakielewa kitu vizuri, weka fedha ili kukikuza zaidi.
Fuata mtiririko huo na utaweza kufanya makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe