3581; Adhabu wanayopata inawatosha.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye safari yako ya mafanikio, unakutana na watu wa aina mbalimbali.
Wapo ambao mambo wanayoyafanya yanakuudhi sana.
Wanakufanya ujisikie vibaya kila unapohitaji kujihusisha nao.
Watu wa aina hiyo huwa wanakufanya ufikirie ni kwa namna gani unaweza kuwaadhibu kwa usumbufu wanaokupatia.
Lakini hayo yote hayana haja, kwa sababu adhabu ambayo tayari wanapata, inawatosha.
Hebu fikiria, wewe unajihusisha na watu hao mara kadhaa tu, lakini wao wanaishi na wao wenyewe mara zote.
Unadhani ni mateso kiasi gani wanayojisababishia wao wenyewe kwa hizo tabia walizonazo?
Unachopaswa kuelewa ni kwamba pale tabia za wengine zinakukera, jua wao wenyewe zinawakera zaidi.
Pale wengine wanapokuumiza, wao wenyewe wanajiumiza zaidi.
Hivyo badala ya kutaka kuwalipa watu kisasi kwa yale wanayofanya, unatakiwa kuwaonea huruma.
Waonee huruma jinsi wanavyojitesa kwa tabia hizo wanazokuwa nazo.
Pia shukuru kwamba wewe haupo kama wao, hujitesi kama wanavyojitesa wao.
Shukuru kwamba watu hao unajihusisha nao kwa vipindi fulani tu na una uhuru wa kutokujihusisha nao kabisa.
Kwa kuwachukulia watu hivyo, hakuna yeyote ambaye ataweza kukusumbua kwa jambo lolote lile.
Rafiki, ni mara ngapi watu wamekuudhi na kutamani kuwaadhibu kwa hayo waliyokufanyia?
Kuanzia sasa tambua tayari wanajiadhibu wao wenyewe kwa hayo wanayofanya hivyo haina haja ya kujisumbua nao.
Mara zote baki kwenye utulivu utakaokuwezesha kufanya makubwa bila ya kujali wengine wanafanya nini.
Waache wengine wajikaange kwa mafuta yao wenyewe. Yale wanayofanya ni adhabu kubwa zaidi kwao wenyewe, huhitaji kuwaadhibu
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe