3582; Kitu muhimu usichoweza kununua.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Kwenye safari yako ya mafanikio, kuna vitu mbalimbali unavyokuwa unahitaji ili kupata mafanikio unayotaka.

Vitu hivyo unaweza kujijengea wewe mwenyewe au unaweza kulipia na ukavipata kutoka kwa wengine.

Ujuzi wa mambo mbalimbali unaopaswa kuwa nao kwenye safari ya mafanikio unaweza kuununua kwa njia mbalimbali.

Unaweza kununua vitabu, unaweza kushiriki mafunzo au unaweza kulipia ushauri kwenye eneo husika.

Lakini kuna kitu kimoja muhimu kwenye safari ya mafanikio ambacho huwezi kukinunua kwa namna yoyote ile.

Kitu hicho ni nidhamu unayohitaji ili uweze kuyafikia mafanikio makubwa unayoyataka.

Huwezi kufundishwa nidhamu,
Huwezi kushauriwa nidhamu,
Huwezi kulazimishwa kuwa na nidhamu.

Nidhamu ni kitu kinachoanzia ndani yako mwenyewe.
Nidhamu huwa inachochewa na hasira ambazo mtu unakuwa nazo juu ya kitu fulani.

Ndiyo maana watu wengi wanaoanzia chini huwa wanapambana sana kufanikiwa.
Lakini wakishafanikiwa wanayapoteza mafanikio hayo kwa kujikuta wanakosa ile nidhamu waliyokuwa nayo.
Hiyo ni kwa sababu hasira waliyokuwa nayo inakuwa imeisha pale wanapopata mafanikio.

Ukitaka kupata mafanikio ambayo yatadumu bila kupotea, unapaswa kuwa na hasira ambayo haiwezi kutulizwa na kitu chochote kile.
Unapaswa kuwa na njaa kali ya mafanikio ambayo haiwezi kushibishwa na kitu chochote.
Unapaswa kuwa mjinga ambaye hakuna wakati unajiona tayari unajua kila kitu.

Kama Steve Jobs alivyowahi kusema, kufanikiwa, baki na njaa na baki mjinga. Hivyo ni vitu viwili vinavyoweza kukupa hasira kubwa ya kuwa na nidhamu ya kuyapambania mafanikio bila kuchoka wala kuridhika.

Kama unajifunza sana kuhusu mafanikio,
Kama unapata sana hamasa ya kufanikiwa,
Lakini unashindwa kudumu kwenye safari ya mafanikio.
Jua unachokosa ni nidhamu.
Na hakuna namna unaweza kujifunza au kununua nidhamu.

Unahitaji kujitengenezea hasira kali ambayo itakusukuma kufanya yote unayopaswa kufanya ili kufanikiwa.
Hasira za matukio huwa zinaisha, hasira ya kufanya makubwa zaidi huwa haiishi.
Kuwa na hasira hiyo na utakuwa na nidhamu ya kukuwezesha kufanya makubwa.

Rafiki, ni mara ngapi umelipia mafunzo ya mafanikio lakini ukashindwa kuchukua hatua unazopaswa kuchukua?
Umeshajua kwamba tatizo siyo kujua cha kufanya. Bali tatizo ni kukosa hasira ya kukusukuma kufanya kwa nidhamu ya hali ya juu sana.
Jenga hasira hiyo ili uwe na nidhamu itakayokupa mafanikio makubwa unayoyataka.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe