3584; Hakuna tatizo jipya.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Huwa kuna kauli inayosema; Hakuna kipya chini ya jua, yote tunayoyaona yalishakuwepo.
Wengi huona kauli hii imekaa kinadharia zaidi, kwa sababu ya uvumbuzi mpya unaofanyika kwenye maeneo mbalimbali.
Lakini ni kauli yenye maana kubwa, kwa sababu licha ya uvumbuzi mpya unaofanyika, bado matatizo ya watu ni yale yale.
Mchumi mmoja wa karne ya 19 alibashiri karne ya 20 watu watakuwa wanafanya kazi nusu ya muda kwa sababu ya uvumbuzi wa teknolojia zinazorahisisha kazi.
Lakini leo tupo karne ya 21 na watu wanafanya kazi muda mrefu kuliko hata huko nyuma.
Hilo linatuonyesha kwamba matatizo yetu binadamu ni yale yale, tangu enzi na enzi.
Pamoja na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, bado matatizo yetu hayajaisha.
Zaidi ni tunapotatua tatizo moja, tunazalisha tatizo jingine linalochukua nafasi ya lile la awali.
Kwa mfano tulikuwa tunapoteza muda mwingi kwenye kazi kwa kukosa teknolojia za kurahisisha.
Sasa tuna teknolojia za kurahisisha kazi na muda unapotelea kwenye teknolojia hizo.
Kuna mambo makubwa matatu ya kujifunza kutokana na hili la kutokuwepo kwa matatizo mapya.
Moja ni njia ya mafanikio ni ya uhakika, kwa sababu mara zote watu wana matatizo. Ukiwasaidia kutatua matatizo hayo, utaweza kupata mafanikio unayotaka.
Na wala hupaswi kuhofia kwamba matatizo ya watu yakiisha na mafanikio yako yanakoma.
Matatizo ya watu yataendelea kuwepo.
Mbili ni kutokata tamaa pale unapoona matatizo hayaishi.
Pale unapotatua tatizo moja halafu likazalisha tatizo jingine, unaweza kuona kama ni kikwazo kwako kufanikiwa.
Lakini ukweli ni hayo ndiyo maisha yenyewe, hakuna siku ambayo hutakuwa na matatizo kabisa.
Kila wakati kutakuwa na matatizo yanayokukabili.
Suluhisho la tatizo ni tatizo jingine linalohitaji suluhisho.
Hivyo ndivyo maisha yalivyo, hayatabadilika kwa ajili yako.
Tatu ni kujifunza kwa wengine pale unapokabiliana na matatizo fulani.
Unapokutana na matatizo, usijaribu kukazana kuyatatua kwa namna yako mwenyewe.
Badala yake angalia wengine ambao walishapitia matatizo kama hayo na jinsi walivyoyatatua.
Utaokoa muda wako mwingi kwa kujifunza kutoka kwa wengine kuliko kujaribu kufanya peke yako.
Na kwa sababu hakuna matatizo mapya, yote unayopitia walishapitia wengine, jifunze kwao ili usipoteze muda.
Rafiki, huwa unafanyaje pale matatizo yanapokuwa hayaishi licha ya kupambana kuyatatua?
Karibu utushirikishe kwenye maoni hapo chini vile umekuwa unachukulia na unavyokwenda kuchukulia sasa baada ya kujifunza hapa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe