3586; Kuna zaidi?
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Imekuwa inasisitizwa sana umuhimu wa kuwa msikilizaji mzuri ili kuweza kuwaelewa wengine na kuwashawishi wakubaliane na wewe.
Lakini kutaka tu kusikiliza inaweza isikusaidie, hasa kama unaowasikiliza hawakupi kile unachotaka.
Njia ya kuwafanya watu wajieleze na wewe usikilize ni kuwauliza maswali.
Binadamu tumezoeshwa kujibu maswali pale tunapoulizwa.
Lakini pia siyo kila maswali yatawafanya watu wajieleze vile unavyotaka.
Mfano ukiwauliza watu maswali ya kujibu ndiyo au hapana, hakuna maelezo mengi utakayoweza kuyapata.
Kuna maswali ya aina mbili ambayo ukiyauliza, watu watajieleza kwako kwa urefu na wewe kupata nafasi ya kuwasikiliza na kuwaelewa vizuri.
Swali la kwanza ni; KWA NINI?
Pale watu wanaposema kitu na unataka kupata ufafanuzi zaidi, waulize kwa nini kisha kaa kimya na sikiliza kwa makini.
Hapo watajieleza kwa kina.
Na kama kwenye kujieleza kwao wamesema kitu ambacho unataka kupata ufafanuzi zaidi, uliza tena kwa nini?
Hakuna ukomo wa kuuliza swali la kwa nini. Kama unamsikiliza mtu vizuri na kuendelea kuuliza, utapata taarifa nyingi kadiri unavyohitaji.
Swali la pili ni; KUNA ZAIDI?
Kama unamsikiliza mtu na unataka kuhakikisha amekuambia kila kilichopo, kuwa unamuuliza kuna zaidi?
Kama ilivyo tabia yetu binadamu ya kujibu maswali tunayoulizwa, kuwauliza watu kama kuna zaidi, watakueleza kama ipo.
Kuweza kuuliza swali hili ni lazima uwe unasikiliza kwa makini, ili unapomuuliza mtu kama kuna zaidi, asukumwe kukueleza zaidi.
Wakati watu wanaanza kukueleza vitu, huwa kuna baadhi ya taarifa wanakuwa hawajapanga kukuambia.
Na hizo zinakuwa ni taarifa muhimu kwako kujua.
Njia ya kupata taarifa zote alizonazo mtu ni kuuliza swali hilo la je kuna zaidi?
Unaposikiliza kwa makini na kuuliza kwa udadisi, watu wanakuwa tayari kujieleza kwako.
Wanajikuta wameshakueleza mpaka mambo ambayo hawakuwa wamepanga kukueleza.
Rafiki, ni mara ngapi umekwama kupata yale uliyotaka kwa sababu kuna taarifa walizokuwa nazo watu na hawakukupatia?
Kuondokana na hilo, kuwa muulizaji mzuri wa maswali na msikilizaji makini.
Kwa kufanya hayo mawili, watu watasukumwa kukuambia kila walichonacho bila ya kuficha chochote.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe