Rafiki yangu mpendwa,
Huwa kuna kauli maarufu inayosema; ‘kukopa harusi, kulipa matanga.’
Wakati wa kuchukua mikopo, watu wengi huwa na furaha kwa kuona wanapata fedha ambazo hawakuwa nazo.
Lakini wakati wa kulipa mikopo hiyo, watu huwa na huzuni, kwa sababu ya gharama zinazokuwa zinaambatana na mikopo hiyo.
Jamii yetu kwa sasa imeandamwa na mikopo mingi ambayo inawaumiza watu wengi. Mikopo hiyo imekuwa inatolewa kirahisi, huku ikiwa na masharti ambayo siyo rafiki kwa wakopaji.
Mikopo hiyo imepewa majina mbalimbali kama kausha damu, vuruga ubongo n.k.
Kwa sababu watu wengi hawana elimu sahihi ya fedha na mikopo, wamekuwa wanaingia kirahisi kwenye mikopo hiyo mibaya ambayo imekuwa siyo msaada bali mzigo kwao.

Benki kuu ya Tanzania (BoT), katika jitihada zake za kutoa elimu sahihi ya fedha kwa wananchi, imeandaa elimu muhimu kuhusu mikopo.
Kwenye elimu hiyo, mimi rafiki yako Kocha Dr. Makirita Amani, ambaye ni mkufunzi wa mambo ya fedha nilipata fursa ya kutoa elimu kuhusu mikopo.
Elimu hiyo kuhusu mikopo imejikita kwenye maeneo ya msingi kama kujua aina za mikopo, sababu za watu kuchukua mikopo, madhara ya mikopo mibaya na hatua za kuchukua ili kuondoka kwenye mikopo hiyo mibaya au kutokuingia kabisa.
Elimu hii imeanza na igizo la mtu aliyechukua mkopo kisha akautumia kufanya sherehe ambayo ilisisimua sana. Lakini baadaye anashindwa kulipa mkopo huo na kupelekea vitu vyake vya ndani kuchukuliwa na nyumba yake kupigwa mnada.
Igizo hilo ndiyo uhalisia wa hali ilivyo kwa wengi kwenye eneo la fedha na mikopo. Wengi wamekuwa wanachukua mikopo na kuitumia kwenye shughuli ambazo siyo za uzalishaji. Matokeo yake wanashindwa kulipa mikopo hiyo na kuishia kupoteza dhamana walizoweka.
Elimu inaendelea na majirani wa aliyepata janga la kupoteza dhamana kutafuta elimu sahihi ya fedha na kisha kwenda kwa mtaalamu ambaye anawaongoza vyema kuhusu mikopo.
Hapo ndipo mimi ninatoa elimu sahihi ya mikopo, ambayo ikifanyiwa kazi itatatua kabisa changamoto za mikopo na kifedha ambazo watu wengi wanapitia.
Elimu hiyo inapatikana kwa njia ya video ambayo ipo kwenye mtandao wa Youtube, unaipata kwa kufungua kiungo hiki; https://www.youtube.com/watch?v=9COhevs23k0
Karibu rafiki yangu uipate elimu hii muhimu kuhusu mikopo na fedha na uache kuwa mhanga wa mikopo mibaya ambayo imekuwa inawakwamisha wengi na kuwarudisha nyuma.
MUHIMU; Kama bado hujaingia kwenye programu ya NGUVU YA BUKU, programu maalumu ya mafunzo na usimamizi wa kufanya uwekezaji kwa vitendo, unapitwa na mengi. Karibu uchukue hatua sasa ya kuingia kwenye programu hiyo ambayo italeta mapinduzi kabisa kwenye maisha yako. Kuingia kwenye programu hiyo, tuma ujumbe NATAKA NGUVU YA BUKU kwenda namba 0756694090 sasa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.