Unawezaje kupunguza upotevu wa muda? Na utumieje muda ambao ungeupoteza kama huna cha kufanya?
   Huu ni mwendelezo wa sehemu ya kwanza ya makala hii(kama hujaisoma itafute uisome).
   Njia kuu ya kupunguza upotevu wa muda ni kuwa na malengo ya muda mfupi na mrefu na kutoyakatia tama. Hapa namaanisha uweke malengo ambayo una shauki kubwa sana ya kuyafikia, na pia uweke mpango wa jinsi ya kufikia malengo hayo. Mpango wa utekelezaji unaweza kuugawa katika mwaka, mwezi, wiki na siku. Hii ina maana kwamba umeshaipanga siku kabla hujaamka, hivyo unapoamka unakuwa tayari unajua nini unakwenda kufanya siku nzima. Kama kweli una shauku kubwa ya kufikia malengo yako na kama una nidhamu binafsi ya kutosha utajikuta unatumia muda mwingi kutekeleza mipango yako. Naomba nisisitize, nidhamu binafsi hapa ni muhimu sana, kwa sababu ni wengi wana mipango ila inawawia vigumu kuitekeleza. Ni vyema kuwa na malengo na mpango wa kufikia malengo hayo ulioandikwa na kuufata. Usijipe sababu za kutotekeleza mpango uliojiwekea mwenyewe.
  Unawezaje kuutumia muda unaoupoteza kama huna cha kufanya? Kuna watu ambao tayari wameshakata tamaa na maisha, wameshakubaliana na matokeo. Labda mtu ameajiriwa kwa muda mrefu na ameshachagua ajira kuwa sehemu ya maisha yake, hivyo kutoka nyumbani saa kumi na moja asubuhi na kurudi saa mbili usiku imeshakuwa kawaida kwake na ni kama sehemu ya maisha yake. Mtu wa aina hii akisoma hapa moja kwa moja anaona nazungumzia kitu ambacho hakimfai, kwamba aokoe muda aufanyie nini? Au ataokoaje muda ama namshawishi aache kazi? Na akishaacha atafanya nini ukizingatia maisha ni magumu na ujasiriamali anauogopa? Ondoa shaka, lengo langu hapa sio kukushawishi uache kazi ama chochote unachofanya kinachokuingizia kipato. Lengo langu ni wewe kujitathmini ni jinsi gani unaweza kutumia muda ambao unapotea.
  Unaweza kuutumia muda unaoupoteza kwa kujiendeleza wewe binafsi. Haijalishi umeajiriwa ama umejiajiri, kwa chochote kile unachofanya unaweza kuweka malengo ya kuwa mtaalamu zaidi, yani kujua zaidi ya unavyojua sasa ama zaidi ya kila mtu anaejua utaalamu huo. Kujiendeleza nakozungumzia sio lazima kwenda darasani, unaweza kujiendeleza kwa kujisomea binafsi, kuzungumza na watu walio katika kada husika na ambao wamefanikiwa ili kujua mbinu gani walitumia kufika hapo walipo. Zama hizi taarifa zinapatikana kwa urahisi kuliko ilivyowahi kuwa, unaweza kujisomea vitabu vya fani uliyonayo ama majarida au hata kutafuta taarifa kwenye mtandao na kuona wenzako duniani wanafanya nini. Unaweza kuwa na vitabu vya kusikiliza(audio books) ambavyo unaweka kwenye simu yako(hata kama ni ya mchina) na kusikiliza ukiwa popote. Kwa mfano muda mwingi unaoupoteza kwenye foleni ambao sio chini ya masaa mawili kwa siku kwa wanaoishi dar unaweza kupata elimu kubwa sana kwa kusikiliza vitabu vilivyosomwa.
   Weka malengo ambayo ungetamani sana kuyafikia, weka mpango thabiti ambao utakusaidia kufikia malengo yako, ugawanye mpango huo kwa mwaka, mwezi, wiki na siku. Ipange siku kabla hujalala hivyo ukiamka unajua ni nini unakwenda kufanya. Malengo yoyote unayoamua unaweza kuyafikia. Acha kupoteza muda, heshimu sana muda kwani ukishapotea haurudi tena.
KAMA UNAHITAJI AUDIO BOOKS BONYEZA HAPA