Kuna usemi unasema “huwezi kuruka na mwewe kama utaendelea kuokoteza na mabata” Usemi huu una maana kubwa sana kwenye maisha na mafanikio. Huwezi kufanikiwa kwa kiwango kikubwa sana zaidi ya watu wanaokuzunguka. Yaani mafanikio yako hayawezi kutofautiana sana na ya watu unaokuwa nao kwa muda mwingi. Watu hao wanaweza kuwa ndugu, marafiki wa karibu, wafanyakazi wenza, wafanyabiahsara wenza na hata kwenye jamii unayoishi. Kuna sababu ya kisaikolojia inayokuridhisha pale unapokuwa juu kidogo ya mtandao wako(watu wote wanaokuzunguka), kama wanaokuona wewe ndio bosi kwao ama wewe ndio umefanikiwa kuliko wao basi moja kwa moja unaridhika nakuona hapo ndio mwisho wa mafanikio. Hii yote inatokana na tabia ya binadamu ya kujilinganisha na wengine. Kama huwezi kujitazama mwenyewe na kutafuta kuufikia uwezo wako ni vigumu sana kutofautiana na wanaokuzunguka.
Kama unataka kufikia mafanikio makubwa kwenye malengo yoyote uliyojiwekea basi inabidi utafute watu wanaoelekea kule unakotaka kuelekea, ama utafute watu waliofanikiwa zaidi ndio ujumuike nao. Simaanishi uwatenge ambao hawajafanikiwa ama hawaonekani kuwa na mlengo wa mafanikio, hapana ila kuwa makini kwenye mambo unayoshirikiana nao. Huwezi kuwatenga kwa sababu wengi ni ndugu zako ama rafiki zako wa karibu, jua ni kitu gani unaweza kuwashirikisha na kitu gani huwezi kuwashirikisha. Watu ambao hawaoni picha kubwa ni vigumu sana kukuelewa utapotaka kuwanesha picha kubwa, mwishowe utajikuta umeshakubaliana nao na kupoteza picha yako. Ni rahisi sana kukubaliana nao kwa sababu mara nyingi ndio unajumuika nao. Ukiweza kuwapata wanaoona picha kubwa ni rahisi kushirikishana nao picha yako. Ukiweza kuwapata waliokwisha fikia mafanikio makubwa itakutia chachu ya kutaka na wewe kuwafikia, ila inabidi uwe makini na kujilinganisha. Usije ukawafikia na ikawa ndio mwisho wa juhudi zako.