Kwa siku za hivi karibuni kumekuwa na matukio mengi ya vijana watanzania kukamatwa na madawa ya kulevya hapa nchini na nje ya nchi. Wengi wamekamatwa na kiasi kikubwa cha dawa hizo ambapo thamani yake ya hela ni kubwa sana. Hebu tujiulize kwa nini haya matukio yanashika kasi kiasi hiki? yani mtu anasikia kabisa kuna mtu kakamatwa na madawa leo ila keshokutwa nae anaenda kufanya hivyohivyo!
Sababu za biashara hii kushamiri ni nyingi, uzembe wa serikali kudhibiti, viongozi wakubwa kujihusisha na hii biashara na maisha magumu ambayo yanasababishwa na serikali!! si ndio? Sasa pamoja na yote hayo kwanini wewe ujihusishe na biashara hii? Kwa nini wewe binafsi ujihusishe na biashara haramu ambayo matumizi yake yanakwenda kuharibu maisha ya binadamu wenzako? Kama maisha magumu ndio yaliyokupeleka kwenye biashara hiyo, je ungekuwa tayari kujiua kwa sababu ya maisha magumu? Kama usingekuwa tayari kwa nini ujihusishe kwenye biashara kama hii?
Kikubwa kinachosukuma watu kukimbilia kufanya biashara hii ni kutaka ‘short cut’ ya mafanikio. Kwa kudhani kwamba kwa kufanya mara moja na kupata fedha nyingi utaachana na biashara hiyo na kufanya nyingine, kosa kubwa. fedha inayopatikana kirahisi hata matumizi yake ni rahisi, ni ngumu sana kuitumia kufanya jambo la maana ndio maana wengi sana hushindwa kuchmoka kwenye hii biashara baada ya kuingia.
Elewa kwamba hakuna njia fupi(‘short cut’) inayoweza kukupeleka kwenye mafanikio ya kweli na yatakayokupatia amani. Njia yoyote fupi itakuingiza kwenye matatiz makubwa na kukuharibia maisha yako. Tumia kipaji, ujuzi na uzoefu wako kutengeneza mafanikio yako ambapo baadae waweza kuyafurahia.