Kuna kitu kimoja amabacho huwa kinawarudisha watu nyuma. Mtu anaweza kuwa ana mipango yake mingi na mizuri tu ila anashindwa kuitekeleza kwa sababu ya kitu hicho. Kila binadamu anakutana na kitu hicho kwenye maisha yake, wachache wameweza kukiepuka ila wengi wameshindwa kukiepuka. Kitu hicho ni HOFU, ni dhahiri kila mtu ana hofu ya kitu fulani. Na kila siku, kila wakati unaambiwa USIHOFU, USIOGOPE lakini bado umejawa hofu na woga. Hata watu ambao unawaona ni jasiri sana na hawaogopi chochote pia wanayo hofu na woga na wamejifunza ama wanajua ni jinsi gani ya kukabiliana ama kutumia vizuri hofu zao.

  Umekuwa unaambiwa mara kwa mara usihofu ama usigope lakini bado umejawa na hofu na woga. Sio kosa lako kushindwa kuondokana na hofu kwa kuambiwa usiogope. Kuambiwa tu usiogope haitoshi kukuondolea hofu. Kuna njia nyingi za kuweza kupunguza ama kundokana na hofu, hapa nitazungumzia baadhi tu ya njia hizo.

1. Tambua hofu na chanzo cha hofu.

  Ni kweli una hofu ila unajua una hofu ya nini? Je unajua ni kitu gani kinasababisha hofu hiyo?

Jambo la kwanza kabisa katika kukabiliana na hofu ni kuitambuna na kuichambua. Jua unahofia nini hasa, jua chanzo kikuu cha hofu yako ni nini. Jua ni mambo gani ukiyafanya yanakungezea hiyo hofu. Pia jua madhara unayoyapata kwa kuwa na hiyo hofu na hatari unayoweza kuja kuipata kutokana na hiyo hofu. Mwisho jua ni matokeo gani maruzi ama faida gani utaipata kama utaweza kundokana na hiyo hofu. Mambo yote hayo yanahitaji kufikiri kwa kina na kuyaandika ili yalete maana zaidi, usifikirie tu juu juu maana kufanya hivyo hutoweza kupata suluhisho la kudumu la hofu yako.

2. Ikabili hofu yako.

  Baada ya kuijua hofu yako na kuichambua sasa weka mipango ya kuikabili. Hofu inaweza kutokana na mambo unayoweza kuyaathiri(yaliyo ndani ya uwezo wako) ama mamb usiyoweza kuyaathiri(yaliyo nje ya uwezo wako)

  Kwa mambo unayoweza kuyaathiri ikabili hofu yako mara moja. Kama kuna jambo unaahirisha kila mara kulifanya kwa kuogopa kushindwa basi anza kulifanya hilo jambo na ulifanye mara nyingi mpaka itakuwa tabia.

  Kwa mambo usiyoweza kuyaathiri ni vyema kuamua kuachana nayo na kutoyafikiria kabisa. Kubaliana na nafsi yako kwamba ndivyo mambo yalivyo na hata ukihofu bado hakuna kitakachobadilika.

3. Badili mtizamo wako juu ya hofu.

  Kubadili mtazamo wako juu ya hofu kunaweza kukusaidia kuikabili hofu kwa urahisi sana.

  Unaweza kuifanya hofu yako kuwa chachu ya wewe kufanya jambo. Kama kuna kitu unaogopa, baada ya kukijua na kujua mdhara ya hofu yako na faida za kundokana na hofu hiyo unaweza kutumia hiyo hofu kama changamoto ya wewe kufanya mambo fulani. Uwepo wa hofu unakufanya ufanye jambo ili kuondokana na hofu.

  Pia unaweza kuitumia hofu kama fursa, hofu inaweza kutumika kama chombo cha kujua matatizo yanayotukabili na jinsi ya kuyatatua. Unaweza kutumia hofu kama mwongozo wa kukufikisha kwenye suluhisho la tatizo linaloleta hofu hiyo. Ili kuweza kuitumia hofu kwa njia hizi ni lazima uwe umeshaitambua na kuichambua hofu yako.

  Hofu ni mbaya, ila kama ukiweza kuitambua na kuichambua hofu inayokukabili yaweza kuwa baraka kwako. Usikae tu na kujilaumu kwa kuwa na hofu ama woga fulani, uchambue huo woga na uone jinsi unavyweza kunufaika na woga ama hofu hiyo.