Kwenye zama za sasa, ambazo ni zama za taarifa, mambo yanabadilika kwa haraka sana. Vitu ni vingi na vinabadilika kwa kasi ya ajabu. Mambo yaliyokuwa yanaonekana ya maana miaka mitano iliyopita leo hii yanaonekana ya kawaida sana. Hivyo ili kwenda sawa na zama hizi za taarifa ni lazima kupata taarifa sahihi kwa wakati sahihi.

  Tunapata tarifa kwa njia ya kujifunza, ila haitoshi tu kujifunza mara moja bali ni kuendelea kujifunza kila siku na kila mara. Kujifunza mara moja haitoshi, lazima kujifunza kuwe endelevu ili kuweza kuendana na kasi hii ya mabadiliko ya taarifa. Usitegemee unachokijua kwa sasa bali kuwa na kiu ya kujifunza mengi zaidi.  Jifunze jifunze jifunze, fanya maisha kuwa darasa na utayafurahia daima na kufikia malengo yako.

  Tofauti na mambo mengine kwenye maisha ambapo kama huendi mbele unaweza kuwa umesimama tu ama unarudi nyuma, kwenye kujifunza kama huendi mbele basi unarudi nyuma, hakuna kusimama. Kama umejifunza jambo fulani na kisha kuacha kujifunza ni dhahiri kwamba muda unavyokwenda ulivyokuwa unavifahamu vinakuwa vinapungua, na vile ulivyonavyo vinakuwa vimeshakosa thamani. Hivyo ni muhimu kuendelea kujifunza kila mara ili kutoachwa nyuma na kasi ya mabadiliko.