Katika jambo ambalo huwa linalalamikiwa sana ni muda, kila mtu analalamika hana muda, yuko ‘bize’. Ukiangalia siku zote ziko sawa, yaani kila siku ina saa ishirini na nne na kila mtu anazo sawa. Wachache wanatumia muda wao vizuri ila wengi wanalalamika muda hautoshi.

  Muda ni kitu ambacho kina wapa watu wengi sana changamto kukitumia vizuri. Watu wote wanaolalamika hawana muda wa kutosha ama wako ‘bize’ ni watumiaji wabaya wa muda. Kama muda ukitumika vizuri bila ya kupotezwa basi kila mtu atakuwa na muda wa kutosha na hakuna atakaekuwa bize. Ili kuufurahia muda ni lazima kuutumia muda vizuri na kwa uangalifu.

  Zifuatazo ni baadhi ya njia zitakazokusaidia kutumia muda vizuri.

1. Weka mpango wa muda wa kila unachotaka kukifanya. Katika malengo yako na mipango yako panga muda wa kufanya kila jambo. Jua ni lini utafanya jambo fulani na itakuchukua muda gani kumaliza. Ni vizuri ukaandika mahali ili ikupe maana zaidi.

2. Pangilia siku yako nzima. Hakikisha kila siku yako imeipanga vizuri kabla ya kuianza, jua jambo gani utalifanya saa ngapi na itakuchukua muda gani kukamilisha.

3. Weka muda wa kupumzika. Kila siku tenga muda wa kupumzika, hii itakufanya usichoke sana hivyo kuweza kukamilisha mipango yako ya siku hiyo.

4. Fanya kila jukumu ulilopewa ama ulilojiwekea kwenye muda uliotolewa. Hapa ndio pagumu sana, kwa sababu watu wengi huwa wanasubiri tarehe ya mwisho ya kukamilisha jukumu ‘deadline’ ndio wanaanza kuhangaika kukamilisha. Muda wa kufanya jambo unaweza kuwa wiki mbili, wengi hawafanyi lolote ila zinapofika siku mbili kabla ya muda kuisha ndio utaona wengi wanahangaika na kulalamikia muda. Kama ukiweza kuyakamilisha majukumu mapema yanapotolewa basi hutopata usumbufu huu wa ‘deadline’

5. Usipoteze muda wako kufanya jambo ambalo halipo kwenye mipango yako. Kwa mfano upo ofisini na una ratiba ya kufanya jambo fulani halafu anatokea mwenzako na kuanza kuleta story za mambo mbalimbali, kumfukuza huwezi kwa sababu ni mtu wako wa karibu hivyo unaanza kupiga story na kuacha kufanya ulilokuwa unafanya. Hii inatokea kwa wengi sana, jifunze kumweleza mtu ukweli hata kama utamuuma. Mwambie sasa hivi kuna jambo unafanya hivyo utamtafuta baadae kwenye muda wako wa kupumzika.

  Hizo ni baadhi ya njia ambazo ukianza kuzitumia sasa utakuwa na muda mwingi mpaka utajishangaa. Sio rahisi kufanya ila ukiamua kufanya inawezekana. Amua kuutumia muda vizuri ili uishi kwa furaha na kupata mafanikio.