Wote tunajua malaria ni hatari na ni moja ya magonjwa yanayoongoza kwa kusababisha vifo hasa kwa watoto wadogo na mama wajawazito. Na pia unajua njia kuu ya maambukizi ya ugonjwa huu ni kwa kuumwa na mbu jike aina ya anofelesi. Na pia umeambiwa njia mojawapo ya kujikinga na maleria ni kuepuka kuumwa na mbu hawa kwa kulala kwenye chandarua chenye dawa ya kufukuza mbu. Ndio yote uliyoambiwa ni sahihi kabisa ila kuna moja la msingi ambalo hujaambiwa ama husikii mara kwa mara. Kuna watu wanaowavutia sana mbu kushinda watu wengine, unaweza kuwa wewe hivyo endelea kusoma ujue kama ni mmoja wao na njia za kuepuka.
Tafiti mbali mbali zilizofanywa na taasisi mbalimbali za afya duniani zinaonesha kwamba kuna watu wanavutia sana kuumwa na mbu. Baadhi ya sababu ama tabia zinazofanya mtu apendwe sana na mbu ni hizi zifuatazo.
1. Watu wenye kundi O la damu. Tafiti zinaonesha kwamba wetu wenye kundi O la damu wanapendelewa sana na mbu kushinda makundi mengine ya damu.
2. Utumiaji wa pombe. Tafiti zinaonaonesha kwamba watu wanafuatwa sana na mbu baada ya kunywa pombe kuliko kabla ya kunywa pombe.
3. Mwezi unapoandama. Tafiti pia zinaonesha mbu wanakuwa na kiu zaidi ya damu wakati mwezi unapoandama(‘full moon’) au mwezi kamili. Inasemekana wakati huo mbu wanakuwa na uhitaji wa damu mara 500 zaidi ya wakati wa kawaida.
4. Harufu mbaya ya miguu pia inachangia mbu kuvutiwa sana na mtu anaetoa harufu hiyo.
5. Mbu wanapendelea sana kuwauma mama wajawazito mara mbili zaidi ya wanavyowauma wanawake wengine.
6. Mbu pia wanapendelea kuwafuata watu waliovaa mavazi yenye rangi nyeusi ikifuatiwa na rangi nyekundu, kijivu na bluu. Mavazi ya kijani, kaki na njano hayana mvuto kwa mbu.
7. Ufanyaji wa mazoezi pia unaoneza kuvutia mbu kwa asilimia hamsini. Hii inatokana na hewa ya kabondayoksaidi tunayopumua na uchafu unaotoka kwenye jasho kuwavutia zaidi mbu.
Kwa kuyajua hayo sasa jiepushe na mazingira yanayowavutia mbu. Kama una tabia inayoweza kurekebishika(kama harufu mbaya) irekebishe na kama haiwezi kurekebishika(mfano kundi O la damu) basi kuwa mwangalifu unapokuwa sehemu yenye mbu.
Kumbuka hutojikinga na mbu waenezao maleria kwa kulala kwenye chandarua pekee, bali kwa kwa kuwaepuka mbu hawa popote wanapweza kukupata ama kuvutiwa na wewe.