Tatizo lolote linapotokea dawa yake ni kulitatua. Kila mtu anafahamu hilo na tatizo linapotokea kila mtu hujaribu kulitatua. Kuna baadhi ya matatizo yanakuwa magumu sana kutatua, yanawasumbua sana watu na mwisho yanaonekana ni matatizo sugu.
Sababu kuu ya tatizo kushindwa kutatulika sio tatizo lenyewe bali ni tatizo la watatuzi. Wengi wanaokimbilia kutatua tatizo wanaangalia matokeo badaa ya kuangalia chanzo hasa ni nini. Ni rahisi kuangalia matokeo kwa sababu ndio yanaonekana kirahisi, ila kukiangaia chanzo ni vigumu kwa sababu hakiko wazi.
Kujaribu kutatua tatizo kwa kuangalia matokeo ni kupoteza tu muda. Hakuna tatizo lisilokuwa na chanzo, na hakuna tatizo enye chanzo kimoja. Matatizo mengi yanasababishwa na vyanzo vingi vidogo vidogo. Hivyo kutokujua vyanzo vyote pia ni sababu ya kushindwa kutatua tatizo.
Kwa mfano kwa tatizo kubwa la madawa ya kulevya tulilonalo hapa nchini wengi wameelekeza kujua nani anatumia na nani anauza. Lakini tatizo hili lina vyanzo vingi ambavyo vinachangia tatizo kuwa kubwa. Baadhi ya vyanzo hivyo ni;
1. Nani waingizaji na wasambazaji wakuu.
2. Kwanini mtu aamue kufanya biashara hii, yaani awe muagizaji na msambazaji mkubwa.
3. Kwa nini inakuwa rahisi sana kwa madawa kuingia na kutoka.
4. Kwa nini vijana wengi wanashawishika kujihusisha na usafirishaji wa madawa hay.
5. Kwa nini vijana wengi wanaamua kutumia madawa ya kulevya.
Hivyo ni baadhi tu ya vyanzo vichache vya tatizo hili. Hebu jiuize kama madawa yangekuwa yanaingia nchini ila yakakosa wateja tatizo lingekuwa kubwa kiasi hiki?
Utatuzi wa matatizo unahitaji njia mpya ya kuyaangalia matatizo hayo. Tuache kuangalia matokeo ya tatizo na badala yake tujue vyanzo vikuu vya tatizo husika.