Kila kukicha mataifa mbalimbali yanagundua silaha kubwa za kivita. Silaha hizo ni kwa ajili ya kujikinga na maadui. Na hata binadamu kia siku tunatafuta mbinu mpya za kupambana ama kuwamaliza adui zetu. Siku zinavyozidi kwenda maisha ya hapa duniani yanaonekana kuwa hatari kwa sababu ya uadui unaojengeka baina ya watu na baina ya mataifa.
Je kwa kuwa na silaha za kisasa na mbinu mbalimbali ndio kutafanya maisha yetu yawe mazuri? Je kwa kuwakabili na kuwaangamiza adui zetu ndio kutatupatia furaha ya maisha?
Hapana, njia hizo haziwezi kuifanya dunia ikawa sehemu salama ya kuishi. Tumeona mifano kwenye vita vikuu vya dunia vilivyopita watu wengi wasiokuwa na hatia walikufa. Hata sasa tunaona yanayoendelea Somalia, Congo, Sudan, Syria na kwingineko. Ni jana tu serikali ya marekani imetoa tahadhari kwa raia wake wanaosafiri nje ya nchi kuwa makini kwa sababu kuna vitishi vya ugaidi! Hakuna amani na furaha ya kweli inayopatikana kwa mapambano na vita.
Upendo pekee ndio utatupatia amani na furaha ya kweli. Kama kila mtu akimpenda mwezake na kila taifa likapenda mataifa mengine dunia itakuwa sehemu salama sana ya kuishi.
Unafikiri haiwezekani kwa kila mtu kumpenda mwenzake? Inawezekana sana kama kweli kila mtu atahamasishwa na kisha kuchukua hatua ya kusambaza upendo. Anza wewe kwa kumpenda kila anaekuzunguka, sambaza upendo na utashangaa jinsi utakavybadili maisha ya watu.
Watu wengi wanaingia kwenye matatizo na kujikuta kwenye hali ngumu kwa sababu ya kukosa upendo. Wengi wanaofanya uhalifu ukichunguza kiundani unakuta walikosa watu waliowapenda na kuwarekebisha kabla tabia zao hazijawa sugu.
Hakuna mtu anaependa kuwa kahaba ama changudoa ila kwa kukosekana upendo wa kweli baina ya binadamu inapelekea mabinti kujiuza. Ingekuwaje kama wanaowanunua wangeamua kuwasaidia bila kufanya nao mapenzi? Ingekuwaje kama mabinti hawa wangekuwa wamelelewa kwa kufunzwa upendo na wao kutoa upendo kwa wanaowazunguka? Huenda wangekuwa wake wazuri sana.
Kama kweli tungekuwa na upendo wa kweli tusingesikia haya ya ufisadi, rushwa na wizi. Ni binadamu wa aina gani anaediriki kuiba hela za umma huku watu wakifa kwa kukosa huduma za afya? Ni binadamu wa aina gani anaeweza kupokea rushwa na kuruhusu chombo kisichofaa kutoa huduma kwa watu na mwishowe kusababisha vifo? Hakika binadamu yeyote anaefanya hivyo amekosa upendo kwa wenzake na ameamua kuishi kama mnyama.
Kila unapofanya jambo lisilo la upendo kwa binadamu mwenzako jua umechangia kwa kiasi kikubwa kuharibu maisha ya binadamu mwenzako.
Dunia inahitaji upendo zaidi ya kitu kingine chochote, wapende wenzako kwa kuonesha vitendo vya upendo. Onyesha upendo kwa kuwashirikisha ujumbe huu marafiki zako wote kwa email, facebook, twitter na mitandao mingine.